Jul 13, 2018 15:14 UTC
  • Le Drian: Hatumruhusu Trump kuiyumbisha Ulaya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amekosoa siasa za kiuchumi zinazotekelezwa na Rais wa Marekani kuhusiana na Ulaya na kueleza kuwa, Paris haitatoa mwanya kwa Trump kuivuruga Ulaya.

Akizungumza na televisheni ya BFM ya nchini Ufaransa, Jean Yves Le  Drian amesema Rais Donald Trump wa Marekani ameutia hatarini mkataba wa mabadiliko ya tabianchi na kuhatarisha makubaliano ya nyuklia na Iran na  utendaji wa Umoja wa Mataifa. 

Le Drian ameongeza kuwa, Trump anashindwa kustahamili uwepo wa Umoja wa Ulaya na anachukua hatua za kukabiliana na Ulaya katika masuala ya kibiashara kwa lengo la kuziyumbisha nchi za bara hilo. Hata hivyo amesema Ulaya haitakubali kuyumbishwa. 

Vilevile Bruno Le Maire, Waziri wa Fedha wa Ufaransa amekosoa siasa hizo za kiuchumi za Trump na kusema: Marekani ilitoa jibu hasi kwa barua iliyotumwa kwa Waziri wa Hazina wa nchi hiyo msimu uliopita wa machipu  ambayo iliiomba Washington iyaruhusu mashirika ya Ulaya kuendelea kushirikiana kibiashara na Iran kwa mujibu wa sheria. 

Bruno Le Maire, Waziri wa Fedha wa Ufaransa 

Mvutano wa kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani ulipamba moto tangu mwezi Machi baada ya Washington kuweka ushuru wa forodha wa asilimia 25 kwa bidhaa ya chuma na asilimia kumi kwa alumini inayoingizwa kutoka Ulaya.  

Msimamo huo wa Washington umekosolewa na pande za Ulaya huku viongozi wa nchi hizo wakisema kuwa watakabiliana na maamuzi hayo ya kiuchumi ya Donald Trump.

Tags