Rais Donald Trump: Umoja wa Ulaya ni adui wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46807-rais_donald_trump_umoja_wa_ulaya_ni_adui_wa_marekani
Rais Donald Trump wa Marekani ametoa matamshi mapya akiutaja Umoja wa Ulaya kuwa ni adui wa Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 15, 2018 23:41 UTC
  • Rais Donald Trump: Umoja wa Ulaya ni adui wa Marekani

Rais Donald Trump wa Marekani ametoa matamshi mapya akiutaja Umoja wa Ulaya kuwa ni adui wa Marekani.

Trump ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CBS  ambapo ameukosoa Umoja wa Ulaya kwa kuitumia vibaya Marekani katika uga wa kibiashara. Hii ni katika hali ambayo wiki iliyopita rais huyo wa Marekani alitoa matamshi makali akizikosoa nchi wanachama wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO), suala ambalo liliibua hali ya suitafahamu ndani ya muungano huo. Katika matamshi yake ya jana, Trump aliitaja EU kuwa ni rafiki wa karibu wa Russia na kusema kuwa, Russia nayo inajulikana kuwa ni adui. Aidha aliendelea kusema, China nayo ni adui wa kiuchumi na Umoja wa Ulaya, ni adui halisi wa Marekani.

Mvutano unaoendelea kufukuta kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya

Akibainisha kwamba nchi nyingi za Umoja wa Ulaya ni wanachana wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) lakini hazichangii gharama, kwa mara nyingine ameikosoa vikali serikali ya Ujerumani kuhusiana na suala hilo. Akiashiria mradi wa bomba la gesi kwa ajili ya kuidhaminia Ujerumani nishati kutoka nchini Russia, Trump amesema, serikali ya Berlin inaipatia Moscow mabilioni ya Dola, na wakati huo huo inaomba hifadhi ya Marekani dhidi ya Russia. Sambamba na kuutaja muamala huo kuwa wa kuchekesha, amesema kuwa hiyo ni aina ya kujisalimisha Ujerumani mbele ya Moscow.