Raia 14 wa Afghanistan wauawa katika hujuma ya ndege za Marekani
Raia 14 wa familia moja, wakiwemo watoto watatu wameuawa katika hujuma ya ndege za Marekani kaskazini mwa Afghansitan mkoani Kunduz.
Taarifa zinasema mauaji hayo yalijiri Ijumaa katika wilaya ya Chahar Dara katika mashambulizi ambayo imedaiwa yalikuwa yanalenga wanamgambo wa kundi la Taliban,
Awali muungano unaoongozwa na Marekani ulikanusha kuuawa raia katika oparesheni hiyo na kudai kuwa ni wapiganaji wa Taliban waliouawa.
Wakuu wa wilaya hiyo wamesema mashambulizi hayo yamepelekea kuuawa raia na pia baadhi ya maafisa wa serikali wamethibitisha kuwa hujuma hiyo imetekelezwa na ndege za kivita za Marekani. Uchunguzi kuhusu tukio hilo ungali unaendelea.
Mkuu wa Wilaya ya Chahar Dara amelalamika kuwa hakufahamishwa na wakuu wa serikali ya Kabul kuhusu shambulizi hilo kabla halijafanyika.
Umoja wa Mataifa unasema hadi kufikia katikati ya mwaka huu, raia 1,692 walikuwa wameuawa Afghanistan hii ikiwa ni idadi kubwa zaidi tokea mwaka 2009.