Kuendelea siasa za mashinikizo ya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini
Ikiwa ni karibu mwezi mmoja umepita tangu Rais Donald Trump na Kim Jong-un wa Korea Kaskazini wakutane nchini Singapore, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema kuwa, kabla ya kujadiliwa suala la kuondolewa vikwazo dhidi ya Pyongyang, nchi hiyo inatakiwa ipige hatua za kivitendo na kwamba kabla ya hatua hizo kupigwa, mashinikizo zaidi dhidi ya Korea Kaskazini yataongezeka.
Akiashiria juu ya ahadi ya kuvuliwa silaha za nyuklia nchi hiyo amesisitiza kwamba, Kim Jong-un ni lazima atekeleze kauli aliyoitoa kwa walimwengu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani pia ameelezea kuendelea mashinikizo yenye lengo la kuifanya Korea Kaskazini itekeleze majukumu yake. Matamshi ya Mike Pompeo yametolewa katika hali ambayo, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza tarehe 12 Juni mwaka huu na baada ya kukutana na Kim Jong-un nchini Singapore kwamba, mkutano wake na kiongozi huyo kijana ulihitimisha vitisho vya silaha za nyuklia za Pyongyang dhidi ya Marekani. Katika kikao hicho, Kim Jong-un na Donald Trump walitiliana saini mkataba ambao Pyongyang iliahidi kuhitimisha silaha zake za nyuklia na wakati huo huo nayo Marekani ikatakiwa kutoa dhamana ya kiusalama kwa Korea Kaskazini. Wakati akirejea kutoka Singapore, Trump aliandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "Kuanzia usiku huu, Marekani inaweza kupata amani kutokana na uwezekano wa kutokea vita kati ya nchi mbili." Mwisho wa kunukuu.
Pamoja na hayo siku 10 tu baada ya kutolewa maneno hayo, rais huyo wa Marekani akilihutubia bunge la kongresi ya Marekani kwa mara nyingine alirefusha hali ya hatari kuhusiana na Korea Kaskazini, huku muda punde baadaye akianza kuzungumzia juu ya uwezekano wa kutokuwa na natija mazungumzo aliyoyafanya na Kim Jong-un. Hivi sasa pia uhusiano wa nchi mbili umejaa mivutano, huku Washington ikiendelea kurefusha vikwazo na mashinikizo dhidi ya Pyongyang. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa Korea Kaskazini kwa mara kadhaa wamesisitiza kwamba, suala la kuvuliwa silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea, litahitajia kwanza kuondolewa vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini, huku Wamarekani nao wakisisitizia kuendelezwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi hiyo madamu haitokubali kutokomeza kwanza silaha zake hizo. Ukweli ni kwamba kuendelea siasa za kuizidishia mashinikizo serikali ya Pyongyang kunakofanywa na Marekani, kwa mara nyingine kunaonyesha kwamba Trump hajafungamana na ahadi zake kuhusiana na suala hilo, kama ambavyo matamshi yake pia si ya kuaminika.
Hii ni sawa kabisa na kama alivyochukua hatua za upande mmoja za kuiondoa nchi yake katika mitakaba ya kimataifa kama vile, mkataba wa hali ya hewa wa mjini Paris, Ufaransa na kadhalika mkataba wa mapatano ya nyuklia ya Iran JCPOA. Katika uwanja huo hivi sasa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anazungumzia suala la kuzidishwa mashinikizo dhidi ya Korea Kaskazini sambamba na kuzitaka nchi nyingine kushirikiana na Washington katika uwanja huo. Weledi wengi wa masuala ya kisiasa, wanaamini kwamba, hatua ya kuendelezwa mashinikizo juu ya Pyongyang kuna maana ya kufeli kwa mazungumzo yaliyofanyika kati ya Trump na Kim Jong-un nchini Singapore sambamba na kubatilika pia madai ya Trump ya kuvuliwa silaha za nyuklia za nchi hiyo ya Asia. Katika uwanja huo Benjamin Haas, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anaandika: "Kuna viashiria vinavyoonyesha kwamba, siasa za mashinikizo za Marekani zinasambaratisha juhudi za udiplomasia zilizotekelezwa na Kim Jong-un." Mwisho wa kunukuu.