Gazeti la Al-Ahram: Siku zote Trump anaibua mgogoro duniani
Gazeti la Al-Ahram la nchini Misri limeashiria siasa za Rais Donald Trump wa Marekani duniani kwa kuandika kuwa, daima Trump anazusha migogoro duniani.
Gazeti hilo limebainisha kwamba rais huyo wa Marekani daima amekuwa akizishughulisha fikra za walio wengi na masuala mapya. Limeelezea matamshi ya Trump ya hivi karibuni kwamba yuko tayari na bila ya sharti lolote kufanya mazungumzo na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, kiuhalisia matamshi hayo ni kinyume cha misimamo yake ya awali. Hii ni kwa kuwa rais huyo amehusika na kuibua migogoro yote ndani ya Iran.
Kadhalika gazeti la Al-Ahram la nchini Misri limefafanua kuwa, ni hivi karibuni tu ambapo Trump ameiondoa nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya Iran, ambayo yalikuwa yamefikia natija. Limeongeza kuwa, mgogogro wa ndani nchini Marekani na juhudi za Trump kwa ajili ya kuuvuka mgogoro huo ni moja ya sababu muhimu zilizomfanya rais huyo kubadili misimamo yake katika siasa za kigeni. Trump anajaribu kuzipotosha fikra za walio wengi kuhusu kutaka kufanya mazungumzo na Iran katika hali ambayo, hadi sasa bado anaendelea kutoa tuhuma bandia na zisizo na msingi dhidi ya taifa hili.