Magazeti ya Marekani yaingia vitani na Rais Donald Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i47483-magazeti_ya_marekani_yaingia_vitani_na_rais_donald_trump
Zaidi ya magazeti 340 ya Marekani yakiwa na lengo la kukosoa misimamo ya chuki ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo kuhusiana na vyombo vya habari, yamechapisha makala zinazoshambulia na kulaani hatua za rais huyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 16, 2018 09:04 UTC
  • Magazeti ya Marekani yaingia vitani na Rais Donald Trump

Zaidi ya magazeti 340 ya Marekani yakiwa na lengo la kukosoa misimamo ya chuki ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo kuhusiana na vyombo vya habari, yamechapisha makala zinazoshambulia na kulaani hatua za rais huyo.

Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian la nchini Uingereza, Alkhamisi ya leo zaidi ya majarida na magazeti 340 nchini Marekani kwa pamoja yamechapisha makala tofauti katika kukosoa siasa za uhasama za Trump za kuvilenga vyombo vya habari vya nchi hiyo. Siku chache zilizopita gazeti la The Boston Globe lilitoa pendekezo kwa vyombo hivyo vya habari la kuchapisha makala aina moja katika kupinga vita alivyovianzisha Rais Donald Trump dhidi ya vyombo vya habari.

Rais Donald Trump wa Marekani

Marjorie Pritchard, mhariri mkuu msaidizi wa gazeti hilo sambamba na kuashiria matamshi aliyoyatoa rais huyo kuwahusu waandishi wa habari, aliwataka wahariri wakuu wa magazeti yote ya nchi hiyo kuchapisha makala siku ya leo ya tarehe 16 Agosti, kuonyesha radiamali yao dhidi ya kile kilichosemwa kuwa ni 'Vita Vichafu dhidi ya Vyombo Huru vya Habari.'

Magazeti ya The New York Times, The Guardian, Chicago Sun-Times, The Philadelphia Inquirer, Miami Herald na magazeti mengi ya nchi hiyo leo yamechapisha makala dhidi ya Rais Donald Trump. Tangu alipoingia madarakani, na kwa mara kadhaa Trump amekuwa akivishambulia vyombo vya habari vya nchi hiyo huku akitaja habari zake kuwa ni bandia na uzushi.