IAEA: Korea ya Kaskazini haijasimamisha miradi yake ya nyuklia
Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umetangaza kuwa hakuna kiashiria chochote kinachoonyesha kuwa shughuli za nyuklia za Korea ya Kaskazini zimesimamishwa.
Wakala wa IAEA jana usiku ulitangaza katika ripoti yake kuwa kuendelea kuimarishwa miradi ya nyuklia ya Korea ya Kaskazini na matamshi ya Pyongyang kuhusu suala hilo yamesababisha wasiwasi mkubwa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuanzia mwishoni mwa mwezi Aprili hadi Mei mwaka huu kumeshuhudiwa viashiria kuhusu kuendelea shughuli za radioactive katika eneo la nyuklia la Yongbyon.
Ripoti hiyo ya wakala wa IAEA imesisitiza kuwa itakuwa vigumu kupata taarifa kuhusu miradi ya nyuklia ya Korea ya Kaskazini iwapo wakala huo utashindwa kukagua miradi ya nchi hiyo. Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia umekumbusha kuwa mwaka 2009 Pyongyang iliwafukuza wakaguzi wa wakala huo katika kituo cha nyuklia cha Yongbyon; na tangu wakati huo hadi sasa wakaguzi wa IAEA hawajaruhusiwa kuingia Korea Kaskazini.
Yukia Amano Mkurugenzi Mkuu wa IAEA pia amesema kuwa chombo hiki cha usimamizi cha Umoja wa Mataifa kitaendelea kufanya kazi zake za kuisimamia Korea ya Kaskazini kupitia taarifa za vyombo vilivyo wazi na kwa picha za satalaiti. Amano anatazamia kuwasilisha ripoti hiyo mwezi Septemba katika kikao cha Bodi ya Magavana wa IAEA.
Ripoti hiyo imetolewa wakati ambapo Rais Donald Trump wa Marekani na Kim Jong-Un kiongozi wa Korea ya Kaskazini siku kadhaa zilizopita walikuwa na mazungumzo huko Singapore ambapo Trump alidai kuwa Korea ya Kaskazini imebainisha azma yake ya kuhakikisha kuwa eneo la Peninsula ya Korea linasalia pasina silaha za nyuklia.