Newsweek: Mchakato wa kumuuzulu Trump unakaribia zaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i47627-newsweek_mchakato_wa_kumuuzulu_trump_unakaribia_zaidi
Jarida la Newsweek la Marekani limeandika ripoti kuhusu uamuzi wa mahakama ya nchi hiyo uliyompata na hatia mwenyekiti wa zamani wa timu ya kampeni za uchaguzi ya Rais Donald Trump na hatua ya wakili wa zamani wa kiongozi huyo ya kukiri kufanya makosa kadhaa na kusisitiza kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa kusailiwa na kuuzuliwa Trump.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 23, 2018 02:39 UTC
  • Newsweek: Mchakato wa kumuuzulu Trump unakaribia zaidi

Jarida la Newsweek la Marekani limeandika ripoti kuhusu uamuzi wa mahakama ya nchi hiyo uliyompata na hatia mwenyekiti wa zamani wa timu ya kampeni za uchaguzi ya Rais Donald Trump na hatua ya wakili wa zamani wa kiongozi huyo ya kukiri kufanya makosa kadhaa na kusisitiza kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa kusailiwa na kuuzuliwa Trump.

Jarida la Newsweek ambalo limezungumzia kwa mapana matukio ya sasa kuhusu faili la Paul Manafort, mwenyekiti wa zamani wa timu ya kampeni za uchaguzi ya Donald Trump na vilevile wakili wake wa zamani, Michael Cohen limetahadharisha kuwa, kuna uwezekano Wademokrati wakadhibiti Kongresi ya Marekani na hatimaye kumuuzulu Rais wa nchi hiyo.

Jarida hilo la Marekani limongeza kuwa, baada ya kusikilizwa kesi ya  Michael Cohen na Paul Manafort kuna uwezekano mkubwa wa kusailiwa na kuuzuliwa Donald Trump kabla ya kukamilisha kipindi chake ya urais. 

Jarida la Newsweek limeripoti kuwa, vilevile kuna uwezo mkubwa wa kushindwa Warepublican katika uchaguzi wa Kongresi wa tarehe 6 Novemba, suala ambalo litakuwa na taathira kubwa katika kadhia ya kuuzuliwa Trump. 

Michael Cohen

Mkuu wa zamani wa timu ya kampeni za uchaguzi ya Donald Trump, Paul Manafort Jumanne iliyopita alipandishwa kizimbani na kupatikana na hatia 8 zinazohusiana na uhalifu wa kibenki na kifedha.

Wakati huo huo wakili wa zamani wa Donald Trump, Michael Cohen alifikishwa mahakamani mjini New York na kukiri makosa 8 yakiwemo ya kukwepa kulipa kodi, utapeli, kukusanya michango ya kampeni za uchaguzi wa rais zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa na kupokea fedha zisizo halali kwa ajili ya timu ya kampeni za uchaguzi wa rais ya Donald Trump.