Majibu ya Russia kwa vikwazo vipya vya Marekani
Kwa miaka kadhaa sasa uhusiano wa Marekani na Russia umekuwa katika mkondo wa mzozo na mivutano.
Mzozo baina ya nchi mbili hizi umechukua mkondo mpana zaidi na licha ya madai ya Rais Donald Trump wa Marekani kwamba, anataka kuboreshwa uhusiano kati ya nchi yake na Moscow, lakini muundo wa kiutawala wa Marekani unataka kuamiliana kwa kuikomalia zaidi Russia. Hii ni sera ya Washington ambayo Trump naye kama Rais wa Marekani amekuwa akiifuata na kuitekeleza.
Moja ya upande muhimu wa Marekani wa kuamiliana na Russia ni kuiwekea vikwazo Moscow kwa visingizio hivi na vile. Katika hatua ya hivi karibuni kabisa, Wizara ya Hazina ya Marekani Jumanne iliyopita ilitangaza kuwawekea vikwazo shakhsia wawili wa Kirusi, mashirika manne na meli sita za Russia kwa madai ya kufanya biashara na Korea Kaskazini na kile kilichotajwa kuwa kukiuka vikwazo vya kimataifa.
Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia anasema kuwa, vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Russia vinatokana na madai yasiyo na maana wala msingi wowote ya udukuzi na kuidhaminia Korea Kaskazini bidhaa za nishati ya mafuta na Moscow itatoa majibu kwa hatua hizo za Washington. Wizara ya Biashara ya Russia imetangaza kuwa, imetoa majibu kwa vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Moscow. Inavyoonekana ni kuwa, kama ilivyokuwa huko nyuma Marekani inataka kuendeleza siasa zake kutumia vikwazo na kuishinikiza Russia ikitumia visingizio mbalimbali.
Lengo la Marekani ni kuifanya Russia ilazimike kuyakubali matakwa ya Washington. Hili ndilo jambo ambalo lilisisitizwa pia na Donald Trump hivi karibuni. Trump alisema kuwa, hana nia ya kuondoa vikwazo dhidi ya Russia na kwamba, atalifanya hilo endapo tu Moscow itachukua hatua ambazo zitakuwa kwa maslahi ya Washington. Rais Donald Trump amesisitiza mara kadhaa kwamba, hakuna mtu aliyeikomalia Russia kama anavyofanya yeye.
Trump ametangaza vikwazo dhidi ya Russia katika fremu ya siasa za Washington dhidi ya Moscow. Mwaka 2011 Marekani ilianza kutekeleza vikwazo dhidi ya Russia katika fremu ya 'Sheria ya Magnitsky' na kuanzia mwaka 2014 baada ya kuibuka na kushadidi mgogoro wa Ukraine serikali ya Marekani iliiwekea vikwazo vya vifurushi kadhaa vya kifedha na kiuchumi Russia.
Aidha Agosti mwaka jana Rais wa Marekani alitia saini 'Sheria ya CAATSA' dhidi ya Russia ambayo ilikuwa na vikwazo vipya na vyenye wigo mpana zaidi dhidi ya Moscow.
Viongozi wa Russia wamesisitiza mara chungu nzima kwamba, lengo la vikwazo hivyo vya Marekani hususan katika sekta ya nishati ni kubana na kubinya uwepo wa kiuchumi wa Moscow katika soko la Ulaya ambapo filihali Russia ina hisa zaidi ya asilimia 30 katika soko hilo.
Hatua ya Marekani ya kupinga kuanzishwa bomba la gesi la Nord Stream-2 kupitia Bahari ya Baltic na kutishia kuweka vikwazo katika uwanja huo inalenga kujiandalia mazingira ya kuuza nishati yake kwa nchi za Ulaya na kwa namna fulani ichukue usukani na nafasi ya Russia ya kudhamini nishati ya gesi barani Ulaya.
Kwa muktadha huo ni jambo lilowazi kwamba, moja ya malengo ya Washington ya kuiwekea vikwazo Russia ni kujipatia fursa ya manufaa ya kiuchumi. Inaonekana kuwa, kwa Marekani wenzo mkuu unaotumiwa na nchi hiyo kwa ajili ya kutwisha malengo yake ya kisiasa, kiuchumi na hata ya kijeshi ni kuyawekea vikwazo mataifa mbalimbali ya dunia.