Sep 25, 2018 02:21 UTC
  • Kushindwa siasa za Marekani duniani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo ameiambia televisheni ya CNN kwamba serikali ya Donald Trump imefeli na kushindwa katika jitihada zake za kuboresha uhusiano wa Marekani na Russia.

Pompeo amesema kuwa: "Suala hilo linavunja moyo sana kwa sababu kuna maeneo ambako Marekani na Russia zina maslahi ya pamoja. Mimi nimeshirikiana nao katika suala la kupambana na ugaidi na kuna maeneo mengine duniani ambako tuna maslahi ya pamoja na Warusi."

Maneno hayo ya Mike Pompeo yametolewa katika hali ambayo mwezi uliopita Washington ilianza kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya Moscow kwa kisingizio kwamba, Russia ilihusika katika jaribio la kutaka kumuua jasusi wa zamani wa nchi hiyo, Sergei Skripal na binti yake, Yulia katika ardhi ya Uingereza.

Matamshi na mienendo ya viongozi wa Marekani kuhusu Russia, kama ilivyo misimamo ya nchi hiyo kuhusiana na nchi nyingine nyingi duniani, ni ya kindumakuwili na yenye migongano. Kwa mfano tu, Washington inadai kuwa inataka kuboresha uhusiano na Russia na wakati huo huo kivitendo inaiwekea vikwazo vipya nchi hiyo kwa kutumia visingizo visivyo na mashiko na madai ambayo hayajathibitishwa kama madai ya jaribio la mauaji ya Sergei Skripal au kwamba iliingilia zoezi la uchaguzi wa rais nchini humo. 

Sergei Skripal na binti yake, Yulia.

Mwenendo kama huo wa Marekani si kuhusiana na Russia pekee bali imekuwa na mienendo kama hiyo pia hata dhidi ya waitifaki wake wakubwa; suala lililoitumbukiza nchi hiyo katika matatizo makubwa na washirika wake wa Ulaya na Canada. Vita vya kibiashara vya Marekani dhidi ya nchi za Ulaya na vikwazo vyake dhidi ya nchi na makampuni yanayoshirikiana kibiashara na Iran ni mfano wa mienendo hiyo ya Marekani. Sera na siasa hizi zimeifanya Marekani itengwe na kubakia peke yake katika uga wa kimataifa.

Wataalamu wa mambo wanaamini kuwa, sera na stratijia hizi za Marekani haziwezi kufanikiwa katika kipindi cha muda mrefu na hatimaye zitakabiliana na matatizo mengi ya kisiasa kiuchumi. Kwa sasa Marekani inafanya mikakati ya kudumaza na kuzorotesha uchumi wa nchi mbalimbali duniani kwa kutumia sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja, kwa sababu ukweli ni kwamba, ustawi wa uchumi wa Marekani katika kipindi cha utawala wa Donald Trump umedorora zaidi kuliko kipindi cha rais yeyote mwingine wa Marekani tangu baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

Donald Trump na Rais wa China Xi Jinping.

John Ross ambaye ni mjumbe wa ngazi za juu katika Taasisi ya Chong Yong ya Chuo Kikuu cha Renmin nchini China anasema: "Siasa na sera za Marekani hazina jambo lolote chanya na nchi hiyo haiwezi kuzuia mwendo wa kinyonga wa ustawi wa uchumi wake kwa kipindi kirefu."

Marekani imekuwa ikiingilia masuala ya kijeshi, kiulinzi na kiuchumi ya nchi mbalimbali na inaonekana kuwa, serikali ya Donald Trump inadhani kuwa, ulimwengu haupaswi kuendeshwa tena kwa mujibu wa mahusiano baina ya nchi huru na zinazojitawala, bali kwa mujibu wa matakwa na amri zake. Jambo hili litakuwa na matokea mabaya kwa Marekani kwa sababu nchi nyingine duniani hazikubaliana na sera hizo, na misimamo kama hiyo ya kijuba itazidi kuifanya Marekani itengwe duniani katika masuala ya kimataifa.     

Tags