Waisraeli 2,700 wajeruhiwa katika mashambulizi ya kisasi ya Iran
Ripoti ya Wizara ya Afya ya utawala wa Kizayuni wa Israel imesema Waisraeli zaidi ya 2,700 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaliyoanza Februari 28.
Ripoti hiyo ambayo haijatoa maelezo yoyote kuhusu idadi ya Waisraeli waliouawa katika hujuma hizo imesema kuwa, walowezi wa Kizayuni wapatao 179 wamejeruhiwa na kulazwa hospitalini katika mashambulizi hayo ndani ya saa 24 zilizopita.
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kuwa, Waisraeli katika mji wa Tel Aviv na katika mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu hawapati hata lepe la usingizi kutokana na milio ya kuogofya ya makombora ya Iran, sanjari na sauti za ving'ora vya tahadhari.
Vita hivi vya kulazimishwa, vilivyoanza asubuhi ya tarehe 28 Februari sawa na 10 Ramadhani kufuatia shambulio la kigaidi la Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vinaendelea huku adhabu dhidi ya wavamizi ikiendelea kubaki katika ajenda kuu ya vikosi vya ulinzi vya Iran.
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu limeendelea kutwanga vituo muhimu vya Israel, ambapo hivi karibuni lilitekeleza shambulio la droni au ndege ya kivita isiyo na rubani dhidi ya kituo cha kijeshi cha Palmachim pamoja na makao ya shirika la ujasusi la Shin Bet ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Operesheni ya Ahadi ya Kweli ya Iran ya kulipiza kisasi inajiri huku Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ikiendelea kushambulia ngome za utawala haramu wa Israel kaskazini na katikati mwa ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel).