Oct 04, 2018 06:53 UTC
  • Vitisho visivyo na kifani vya Marekani dhidi ya Russia

Uhusiano wa Russia na Marekani umekuwa wa mivutano na migogoro ya mara kwa mara katika miaka ya hivi kaibuni. Maslahi yanayongongana ya madola hayo mawili makubwa katika nyanja za kiuchumi, kijeshi, kiusalama na sekta ya nishati yamewafanya Wamarekani waitambue Russia kuwa ni adui mkubwa zaidi wa serikali ya Washington katika masuala ya kijeshi na kiusalama na tishio nambari moja la nyuklia kwa Marekani.

Hata hivyo hatua hizo za kiuhasama za Marekani dhidi ya Russia hazikunyamaziwa kimya na Moscow ambayo pia kwa upande wake imeitambua serikali ya Washington kuwa ni tishio kubwa. Suala hili sasa limechukua mkondo mpya na Washington imechukua msimamo usiokuwa na kifani na kutishia kuishambulia Moscow. Marekani imetishia kuwa, iwapo italazimu itashambulia na kuangamiza mitambo ya makombora ya Russia. Balozi wa kudumu wa Marekani katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) Kay Bailey Hutchison Jumanne ya wiki hii aliituhumu Russia kuwa inastawisha kwa siri mfumo wa makombora yaliyopigwa marufuku ya Cruise na kutishia kwamba, Washington itashambulia na kuharibu mfumo huo kabla haujaanza kufanya kazi. Hutchison amesema Washington ingali inataka kutatuliwa kadhia hiyo kwa njia za kidiplomasia lakini iwapo Moscow itaendelea kustawisha mfumo huo wa makombora ya masafa ya kati, Marekani iko tayari kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Russia.

Kay BaileyHutchison

Marekni inadai kuwa, Russia inastawisha mfumo wa makombora unaokiuka makubaliano ya nyuklia kati ya pande hizo mbili yaliyotiwa saini katika kipindi cha Vita Baridi yaani makubaliano ya INF ambao utaiwezesha Moscow kuzishambulia nchi za Ulaya kwa silaha za nyuklia katika kipindi kifupi. Hata hivyo Russia imekuwa ikipinga madai hayo. Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa, taarifa iliyotolewa na balozi wa Marekani katika shirika la NATO akidai kwamba serikali ya Russia inapaswa kusitisha ustawishaji wa siri wa mtambo wa makombora yaliyopigwa marufuku ya Cruise la sivyo Marekani itaushambulia na kuuangamiza kabla haujaanza kutumika, ni ya hatari sana. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova amesema kuwa: Inaonekana kwamba watu wanaotoa matamshi kama haya hawaelewi kiwango cha majukumu yao na na hawajui hatari ya lugha yao ya hujuma. 

Maria Zakharova

Siku chache zilizopita pia Waziri wa Mambo ya Ndani wa Marekan, Ryan Zinke alisema kuwa, jeshi la majini la nchi hiyo linaweza kuiwekea Russia mzingiro wa baharini ili kuizuia kuingilia masoko ya nishati ya Mashariki ya Kati. Russia imetaja hatua kama hiyo kuwa itakuwa sawa na tangazo la vita.

Hapa shaka kuwa, misimamo hiyo ya viongozi wawili wa ngazi za juu katika serikali ya Marekani dhidi ya Russia ambayo imeelezwa kwa mara ya kwanza kabisa katika kiwango hicho, haiwezi kuchukuliwa bila ya kujadiliwa kati ya viongozi wa juu kabisa wa serikali ya Washington na inaweza kutambuliwa kuwa ni ishara ya mipango kabambe ya serikali ya Marekani dhidi ya Russia ya kutaka kubana uwezo wa Moscow katika masuala ya makombora na nishati.

Trump, Kay Bailey Hutchison na maafisa wengine wa ngazi za juu wa Marekani.

Inaonekana kuwa, hitilafu za pande hizo mbili na kiwango cha mivutano yao vinaelekea upande wa mpambano na makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi, au kwa maneno mengine vita kati ya madola hayo mawili makubwa yanayomiliki silaha za nyuklia. Hii ina maana kwamba, Washington imechukua hatua kubwa ya kukabiliana na Moscow katika masuala mbalimbali hususan katika medani za kijeshi na masuala ya nishati.

Pamoja na hayo yote tajiriba ya huko nyuma inaonesha kuwa, Russia haitakaa kimya na itachukua hatua za kujibu mapigo kwa njia na mbinu zake. Kuendelea kwa mwenendo huo kuna maana ya kujitokeza hali ya ukosefu wa utulivu na amani katika uga wa kimataifa kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha baada ya Vita Baridi.

Tags