JCPOA, fursa kwa ajili ya kujitegemea kifedha Ulaya
(last modified Sun, 07 Oct 2018 02:26:28 GMT )
Oct 07, 2018 02:26 UTC
  • JCPOA, fursa kwa ajili ya kujitegemea kifedha Ulaya

Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akikosoa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambayo yalifikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 ikiwemo na Marekani yenyewe na kuyatataja makubaliano hayo kuwa ndiyo mabaya zaidi kuwahi kufikiwa.

Hatimaye Trump tarehe 8 Mei mwaka huu alitangaza habari ya kujiondoa Marekani katika makubaliano hayo ya nyuklia na kuiwekea tena Iran vikwazo vya nyuklia. Mkabala wake nchi za Ulaya zinasisitiza udharura wa kulindwa makubaliano ya JCPOA kwa ajili ya maslahi yao na ndio maana Iran na Umoja wa Ulaya katika miezi kadhaa ya karibuni zikafanya mazungumzo yenye lengo la kudumisha makubaliano hayo baada ya Marekani kujitoa. Umoja wa Ulaya ambao nchi zake 3 zinazounda Troika ya Ulaya yaani Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ambazo ni wananchama wa kundi la 5+1, umeunga mkono makubaliano hayo ya nyuklia na kusisitiza udharura wa kukabiliana na hatua za Marekani za kutaka kuyafuta. Nchi hizo zimechukua hatua kadhaa ili kukabiliana na hatua za Marekani katika uwanja huo. Kama alivyosema Bi Federica Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya: Ushirikiano wetu na nchi wanachama na washirika wengine duniani unaendelea ili  kuhakikisha kuwa,  Iran na watu wake wananufaika na uhusiano wa kiuchumi na nchi za Ulaya na nyingine za dunia.

Bi Federica Mogherini, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya 

Katika mazungumzo yake na Iran, Umoja wa Ulaya uliahidi kwamba utawasilisha kwa Tehran kifurushi cha kuyalinda makubaliano hayo ya JCPOA na kukabiliana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Kuhusiana na suala hili, Umoja wa Ulaya tayari umewasilisha sheria kadhaa za kukabiliana na athari za vikwazo vya Marekani ili kuiunga mkono Iran na mashirika ya Ulaya mkabala na vikwazo vya Marekani. Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, sheria hizo kivitendo haziwezi kuzuia kuondoka Iran mashirika makubwa ya Ulaya. Hatua nyingine iliyochukuliwa na Ulaya ni kuanzisha taasisi ya fedha inayojisiamamia bila ya kuitegemea Marekani ili kabla ya mwezi Novemba mwaka huu yaani muhula ulioainishwa na Marekani kwa ajili ya kuiwekea Iran vikwazo vipya iweze kulinda uhusiano wake wa kibiashara na Tehran. Kuhusiana na suala hilo, Bruno Le Maire Waziri wa Fedha wa Ufaransa tarehe 5 Oktoba alivitaja vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran kuwa ni fursa ambayo inaweza kutumiwa na nchi za Ulaya kwa ajili ya kuunda  taasisi huru za kifedha. Le Maire alisema: Binafsi naamini kuwa, matokeo ya mgogoro wa Iran yatakuwa fursa kwa Ulaya kuanzisha taasisi zake za kifedha zinazojitegemea ili kufanya biashara na upande wowote ule. 

Bruno Le Maire, Waziri wa Fedha wa Ufaransa 

Inatazamiwa kuwa, taasisi hiyo mpya haitakuwa benki bali itafanya kazi zake katika kalibu ya sheria na kwa kujitegemea. Lengo la taasisi hiyo ya fedha ni kufanya miamala ya kifedha na Iran kupitia njia za kawaida za kibenki. Taasisi hiyo mpya ya fedha haitatambulika kama benki bali itakuwa taasisi wasita (Special-purpose entity). Nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya zinataraji kunufaika na taasisi hii ya fedha. Kwa utaratibu huo, miamala mingi ya kibiashara, kiviwanda na hata biashara ya mafuta ya Iran na Ulaya itawezekana kupitia taasisi hiyo.

Ni wazi kuwa kitendo hiki cha Umoja wa Ulaya ni hatua yenye lengo la kuziwezesha kifedha nchi za Ulaya na kukata utegemezi wao kwa Marekani. Nchi za Ulaya zimekasirishwa sana na haziridhishwi na hatua za kimabavu na za sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Donald Trump ambaye ametaka kukatwa kikamilifu uhusiano wote wa kibiashara na kifedha kati ya nchi za Ulaya na Iran. Baada ya kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, serikali ya Marekani ilianzisha mikakati na hatua  za kuishinikiza zaidi Jamhuri yya Kiislamu ya Iran na inaendeleza jitihada za kuzishawishi nchi nyingine ziunge mkono vikwazo vyake vya upande mmoja dhidi ya wananchi wa Iran. 

Waziri wa Fedha wa Ufaransa amesema katika uwanja huo kwamba: Marekani haina haki ya kuamua iwapo sisi tunaweza kufanya biashara na Iran au la. Msimamo huu wa Waziri wa Fedha wa Ufaransa unaonyesha namna washirika wa Ulaya wa Washington wanavyopinga sera za kibeberu za Marekani ambazo situ kuwa zimesababisha mivutano na mikwaruzano kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA bali pia katika masuala mengine mengi.  

Tags