Makumi ya wajahiri wahofiwa kufa maji pwani ya Uturuki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i48702-makumi_ya_wajahiri_wahofiwa_kufa_maji_pwani_ya_uturuki
Makumi ya wahajiri wanahofiwa kupoteza maisha baada ya boti yao kuzama katika pwani ya Uturuki ya Aegean.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 10, 2018 10:49 UTC
  • Makumi ya wajahiri wahofiwa kufa maji pwani ya Uturuki

Makumi ya wahajiri wanahofiwa kupoteza maisha baada ya boti yao kuzama katika pwani ya Uturuki ya Aegean.

Gadi ya Pwani ya Uturuki imesema leo Jumatano kuwa, miili tisa ya wahajiri hao imeopolewa majini na kwamba timu ya wapiga mbizi inasaka miili ya wahajiri wengine wasiopungua 25.

Mwanamke mwenye umri wa miaka 30 amesema binafsi alinusurika baada ya kuogolea na kurejea hadi ufukwe wa pwani ya Aegean baada ya boti yao kuzama, ingawaje anasema amempoteza mumuwe na wanawe watano katika ajali hiyo.

Amesema boti hiyo ilizama usiku wa kuamkia jana, muda mfupi baada ya kuondoka katika mji wa Foca, mkoani Izmir ikiwa na wahajiri kati ya 30 na 35.

Miili ya wahajiri ikiopolewa majini

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya wahajiri wengine wasiopungua 34 kuaga dunia baada ya boti yao kupata hitilafu magharibi mwa bahari ya Mediterania, huku wengine 26 wakinusurika kifo. 

Kwa mujibu wa Shirika la Wahajiri la Umoja wa Mataifa IOM, idadi ya wahajiri waliofariki dunia mwaka huu pekee katika Bahari ya Mediterrania wakiwa safarini kuelekea Ulaya ni zaidi ya 1600.