Oct 30, 2018 06:32 UTC
  • Malalamiko ya Moscow kuhusu kuingilia Marekani masuala ya ndani ya Russia

Uhusiano wa Russia na Marekani uko katika hali mbaya zaidi hivi sasa ikilinganishwa na kipindi chote cha baada ya vita baridi. Marekani inatuhumiwa kufanya njama kubwa za kuingilia masuala ya ndani ya Russia. Mwaka 2016 pia, Washington iliamua kuiwekea vikwazo nchi hiyo kwa madai kuwa Moscow iliingilia uchaguzi wa rais wa Marekani.

Hatua hiyo ya Washington imekumbwa na hasira za viongozi wa Moscow ambao wamekuwa wakilalamika muda mrefu kwamba Marekani inaingilia sana masuala yake ya ndani pamoja na kuwachochea wananchi wafanye uasi au maandamano ya kupinga serikali.

Hivi karibuni, Segey Lavrov, waziri wa mambo ya nje wa Russia alisema kuwa, licha ya Marekani kujifanya ina hamu ya kustawisha uhusiano wake na Moscow, lakini inaunga mkono misimamo ya wapinzani ya kuipindua serikali ya Russia kiasi kwamba kila mwaka Washington inatenga fedha nyingi kuendeshea kampeni hiyo ya kiuadui kupitia asasi zisizo za kiserikali. Pia amesisitiza kuwa, viongozi wa Russia wana ushahidi madhubuti unaoonesha namna Marekani inavyoingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Marais wa Russia na Marekani

 

Aidha Lavrov amesema: Wanadiplomasia wa Marekani mara chungu nzima wamekuwa hata wakishiriki katika harakati za wapinzani na maandamano yao ambayo ndani yake wanasema wazi kuwa wana nia ya kupindua serikali n.k.

Hivi sasa kuna idadi kubwa ya taasisi zisizo za kiserikali za Marekani zinazofanya harakati zao ndani ya Russia kwa jina la harakati za kijamii, upashaji habari na kutoa misaada ya kibinadamu wakati ukweli wa mambo ni kuwa, asasi zote hizo zinaendesha harakati za kisiasa.

Taasisi hizo za NGO ambazo aghlabu yake zinaendeshwa na wanasiasa, mabepari na mashirika makubwa pamoja na wabunge wa Congress wa Marekani, zimetengeneza kanali moja tata sana ya kuathiri masuala ya kijamii ndani ya Russia ili wakati wowote itakapohitajika, ziweze kutumika katika masuala kama ya uchaguzi n.k.

Vile vile baada ya kuzuka mivutano kenye uhusiano wa Russia na nchi za Magharibi katika kipindi cha miaka minne iliyopita, hasa kutokana na mgogoro wa Ukraine, Marekani imeamua kutumia fursa hiyo kufanya njama kubwa za kuingilia masuala ya ndani ya Russia kwa ajili ya kuidhoofisha serikali ya Moscow na pia kuufanya utamaduni wa Magharibi uenee na kulidhibiti taifa la Russia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov

 

Marekani inaendesha vita vyake vya kisaikolojia dhidi ya serikali ya Russia kwa mbinu za aina mbili, yaani kwa kutumia vyombo vya habari vya Russia kwenyewe na pia kwa kutumia taasisi za kijamii zisizo za kiserikali za nchi hiyo kueneza utamaduni wa Magharibi hasa kwa jina la demokrasia.

Rais Vladimir Putin amesema kuhusu suala hilo kwamba, asasi za kiraia za madola ya kigeni ni nyenzo zinazotumiwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine duniani. Taasisi hizo zinazodhamiwa kifedha na madola ya kigeni hazifichi tabia yake ya kuingilia masuala ya ndani ya Russia. 

Serikali ya Russia inasema kuwa, upinzani na malalamiko ya ndani ya nchi hiyo yanatokana na uchochezi wa madola ya kigeni; hivyo imeamua kukabiliana na taasisi hizo zinazodhaminiwa kifedha na madola ya Magharibi hasa Marekani kwa kuziwekea sheria za kuzidhibiti. Hivyo mbali na vita vya kiuchumi, kisiasa na kijeshi, hivi sasa tunashuhudia pia vita laini vya kidiplomasia baina ya Russia na Marekani.

Inaonekana Moscow inalitambua vyema jambo hilo na ndio maana imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za ima kuzibana au kuzifungia na kuzipiga marufuku kabisa baadhi ya taasisi zisizo za kiserikali ambazo inahisi zinatumiwa na madola ya kigeni hasa Marekani kuvuruga utulivu na usalama wa Russia.

Tags