Pakistan: Hatubebi dhima ya kushindwa Marekani nchini Afghanistan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ametupilia mbali madai ya Rais Donald Trump wa Marekani kwamba Islamabad inawaunga mkono magaidi na kusisitiza kuwa, Pakistan si tu haibebi dhima ya kushindwa Washington nchini Afghanistan, lakini pia iliongoza juhudi za mwanzo za kutoa mchango chanya wa kuleta amani ndani ya nchi hiyo jirani.
Shah Mehmood Qureshi ameyasema hayo akijibu matamshi ya juzi ya Rais Donald Trump wa Marekani na kuongeza kwamba, dunia inafahamu nafasi chanya ya Islamabad katika vita dhidi ya ugaidi. Amesisitiza kwamba matamshi ya chuki ya rais wa Marekani dhidi ya Pakistan, hayawezi kubadili ukweli. Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ameongeza kwamba, lau kama Pakistan isingeshirikiana na Marekani katika vita dhidi ya ugaidi, basi Washington ingepata hasara kubwa. Aidha Jumatatu ya jana Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan sambamba na kukosoa matamshi ya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya nchi yake alisema kuwa, ni bora Marekani badala ya kuituhumu Pakistan, ikubali kushindwa kwake nchini Afghanistan.
Khan aliashiria kuwa, katika vita dhidi ya ugaidi, Pakistan ilitoa mhanga roho za watu elfu 75 sambamba na kupata hasara ya zaidi ya dola bilioni 123 na kwamba mkabala wake Marekani iliipatia Islamabad msaada wa kiasi cha dola bilioni 20 tu. Jumapili iliyopita, akizungumza na kanali ya televisheni ya Fox News Rais Donald Trump wa Marekani alisema kuwa, licha ya Washington kuipatia misaada ya kifedha Pakistan, lakini nchi hiyo "haijafanya jambo lolote la maana" kwa ajili ya Washington nchini Afghanistan.