UNICEF: Karibu mabarubaru 80 kuangamia kwa Ukimwi kila siku
Vijana wadogo yaani barubaru 76 wanakadiriwa kuwa watafariki dunia kila siku ulimwenguni kote kati ya mwaka huu na 2030 iwapo uwekezaji sahihi hautafanyika kuzuia Virusi Vya Ukimwi, VVU miongoni mwa tabaka hilo la wanadamu.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF iliyotolewa Alhamisi kuelekea Siku ya Ukimwi Duniani tarehe mosi Disemba
Ripoti hiyo ya UNICEF yenye anuani ya, "Watoto, VVU na Ukimwi: Dunia mwaka 2030", inataka uwekezaji zaidi ili wasinyanyapaliwe na wapate huduma zinazostahili.
Henrietta Fore, Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF anasema ripoti inaonesha dhahiri kuwa dunia haiko kwenye njia sahihi katika vita vya kutokomeza Ukimwi miongoni mwa watoto na barubaru ifikapo 2030.

Hata hivyo Bi Fore amesema, kuna matokeo chanya katika programu za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama hadi mtoto lakini haijakwenda mbali zaidi, wakati programu za kutibu VVU na kuzuia kuenea miongoni mwa watoto ni chini ya matarajio.
Matumaini kutoka kwenye ripoti ni kwamba idadi ya watoto na barubaru watakaokufa kutokana na sababu zitokanazo na ukimwi itapungua kutoka 119,000 hadi 56,000 mwaka 2030.
Ripoti imetaja sababu mbili kuu za kasoro kwenye vita dhidi ya VVU miongoni mwa watoto na barubaru, mosi ni upungufu wa kasi ya kuzuia VVU miongoni mwa watoto na kosa la kutoaangazia vichochezi vinavyosababisha hali hiyo kwani kundi hilo la watu hawajui hali yao ya VVU na pili wale wamepatikana kuwa na virusi hivyo na kuanza tiba hawazingatii tiba.
Kwa sasa watoto wadogo na mabarubaru milioni tatu wanaishi na VVU kote ulimwenguni na zaidi ya nusu wako maeneo ya kusini na mashariki mwa Afrika.
UNICEF imesema ili kushinda vita dhidi ya VVU ni lazima kuongeza kasi ya kupunguza maambukizi kwa vizazi vijavyo.