EU yaongeza vikwazo vyake dhidi ya serikali ya Myanmar
Baraza la Umoja wa Ulaya limetoa taarifa na kusema kuwa limeamua kuiwekea vikwazo zaidi serikali ya Myanamar kutokana na ukatili na ukandamizaji iliowafanyia Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Taarifa hiyo ya jana Jumatatu imesema kuwa, kwa kuzingatia uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanyika katika mkoa wa Rakhine wa magharibi mwa Myanmar, baraza hilo limeamua kuwawekea vikwazo zaidi baadhi ya maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi wa nchi hiyo.
Taarifa hiyo ambayo imetolewa sambamba na kikao cha baraza la mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Ubelgiji, imetilia mkazo pia wajibu wa kubuniwa njia maalumu huru ya kuchunguza jinai walizofanyiwa Waislamu hao huko Myanmar.
Hii ni katika hali ambayo, maafisa saba wa ngazi za juu wa kijeshi wa Myanmar wamo katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya. Vikwazo hivyo vinajumuisha kuzuiwa mali za maafisa hao na kupigwa marufuku kutembelea nchi za Ulaya.
Jeshi la Myanmar kwa kushirikiana na mabudha wenye misimamo mikali limefanya ukatili mkubwa wa kupindukia dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Tangu tarehe 25 Agosti 2017 hadi hivi sasa, zaidi ya Waislamu elfu sita wa jamii ya Rohingya wameshauawa na elfu nane wengine wamejeruhiwa mbali na milioni moja waliokimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya jeshi la Myanmar na mabudha wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu hao.