Mogherini: EU haitairuhusu Marekani iingilie uhusiano wake na Iran
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema Marekani haiwezi na haipaswi kuitwisha EU sera zake na kwamba umoja huo wenye nchi wanachama 28 hautairuhusu Washington iufanyie maamuzi juu ya uhusiano wake wa kibiashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Tovuti ya Livemint imemnukuu Federica Mogherini akisema hayo katika mahojiano na gazeti la Arab News la Saudi Arabia yaliyochapishwa Jumanne na kuongeza kuwa, EU imejitolea kwa dhati kuendelea kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, licha ya Marekani kujiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa.
Amesema, "Tunafanya kazi kwa pamoja kama umoja wa nchi 28 na kwa ushirikiano wa jamii ya kimataifa ili kuyanusuru makubaliano ya nyuklia ambayo hadi sasa yametekelezwa kikamilifu na kuidhinishwa mara 13 katika ripoti ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Sehemu ya ushirikiano huu ni kuhakikisha kuwa mashirika ambayo yanataka kufanya biashara halali na Iran yanaruhusiwa na kupewa dhamana. Hili ndilo jambo ambalo tunalishughulikia kwa sasa."
Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amekariri kuwa, anatumai kuwa mfumo maalumu kwa ajili ya mabadilishano ya fedha kati ya Iran na Ulaya kwa kifupi SPV utazinduliwa hivi karibuni.
Amesisitiza kuwa, EU haitaruhusu uingiliaji wa madola ajinabi hata yawe ni waitifaki wa karibu wa umoja huo, kuvuruga biashara halali kati yake na Iran.
Itakumbukwa kuwa tarehe 8 Mei mwaka uliomalizika, Rais wa Marekani, Donald Trump aliitoa nchi yake katika mapatano hayo ya JCPOA na kutangaza kuirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyoondolewa baada ya kufikiwa mapatano hayo.