Malaysia haitawaruhusu wanariadha wa Israel kuingia nchini humo
Malaysia imesema haitawaruhusu wanariadha wa utawala wa Kizayuni wa Israel kukanyaga ardhi ya nchi hiyo, ikiwa ni katika mwendelezo wa serikali ya Kuala Lumpur wa kupambana na utawala huo batili.
Waziri Mkuu wa Malysia, Dakta Mahathir Mohammad amewaambia waandishi wa habari kuwa, "Serikali yangu haitatoa kibali cha kuwaruhusu wanariadha wa michezo ya walemavu wa Israel kuingia nchini hapa na iwapo watajileta, tutaihesabu hatua hiyo kama ukiukaji wa sheria."
Dakta Mahathir amefafanua kuwa, Malaysia ni muungaji mkono wa Palestina na wala haina uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel, na kwa msingo huo, serikali yake itakuwa inakiuka sheria iwapo itatoa viza kwa ajili ya wanamichezo hao wa Israel.
Licha ya mashinikizo kutoka kwa Kamati ya Kimataifa ya Paralimpiki na Shirikisho la Olimpiki la Israel ya kuitaka Malaysia iangalie upya uamuzi wake huo, lakini serikali ya Dakta Mahathir imeshikilia kuwa haitawaruhusu wanamichezo hao wa Kizayuni kuingia nchini humo, kushiriki mashindano ya kimataifa ya uogoleaji ya walemavu.
Mashindano ya Mabingwa wa Kuogolea ya Walemavu (World Para Swimming Championships) yanatazamiwa kufanyika kati ya Julai 29 na Agosti 4 mwaka huu, katika mji Kuching, kisiwani Borneo, kusini mashariki mwa Malaysia.
Huko nyuma pia Malaysia ilikataa kuziruhusu timu za tenisi na mchezo wa upigaji makasia za utawala huo wa Kizayuni kuingia katika nchi hiyo kushiriki mashindano ya kimataifa ya michezo hiyo.