Mogherini: Sitokwenda katika kikao cha Warsaw
https://parstoday.ir/sw/news/world-i51035-mogherini_sitokwenda_katika_kikao_cha_warsaw
Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya ametangaza kuwa hatashiriki kikao kilicho dhidi ya Iran kilichoitishwa na Marekani huko Warsaw, mji mkuu wa Poland.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 22, 2019 02:47 UTC
  • Mogherini: Sitokwenda katika kikao cha Warsaw

Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya ametangaza kuwa hatashiriki kikao kilicho dhidi ya Iran kilichoitishwa na Marekani huko Warsaw, mji mkuu wa Poland.

Bi Federica Mogherini alisema jana (Jumatatu) pambizoni kwa kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Ubelgiji kwamba atahudhuria kikao cha Umoja wa Afrika kitakachofanyika Addiss Ababa mji mkuu wa Ethiopia badala ya kushiriki kikao cha huko Warsaw, Poland. 

Itakumbukwa kuwa Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani siku kadhaa zilizopita alisema kuwa Washington ina mpango wa kuitisha kikao dhidi ya Iran katika mji mkuu wa Poland, Warsaw. Kikao hicho ambacho kimeandaliwa chini ya anuani "Mustakbali wa Mashariki ya Kati" kitafanyika tarehe 13 na 14 mwezi Februari mwaka huu. Aghalabu ya nchi siku chache zilizopita zimetangaza kuwa hazitoshiriki kwenye kikao hicho licha ya Marekani kutangaza kuwa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa makumi ya nchi watahudhuria. 

Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani 

Nchi kadhaa kama Ufaransa pia zimetangaza kuwa zitashiriki kwenye kikao cha Warsaw katika ngazi ya chini kabisa. Wakati huo huo Ujerumani na Uingereza bado hazijatangaza iwapo zitashiki katika kikao hicho au la. Gazeti la Wall Street Journal la nchini Marekani limeandika kuwa, nchi za Ulaya hazitajiunga na muungano huo dhidi ya Iran unaofuatiliwa na Washington.