Siku ya Hijabu Duniani yaadhimishwa katika mji mkuu wa Uingereza
Wanawake Waislamu nchini Uingereza wamekusanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, London kuadhimisha Siku ya Hijabu Duniani (World Hijab Day).
Wanawake Waislamu wa London, wamekusanyika katika mji mkuu huo wa Uingereza kwa madhumuni ya kuzungumzia masuala na matatizo mbali mbali ambayo wanawake wanaovaa hijabu wanakabiliana nayo, na vile vile kuongezeka kwa hisia za hofu na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) nchini humo.
Mkusanyiko huo wa wanawake Waislamu ulifanyika kwa mara ya kwanza katika mji mkuu huo wa Uingereza siku ya Ijumaa.
Siku ya Hijabu Duniani iliyoanzishwa rasmi mwaka 2013, huadhimishwa kila mwaka tarehe Mosi Februari kwa lengo la kufuta na kuondoa mazoea hasi yaliyoenea kuhusu wanawake Waislamu wanaovaa hijabu.
Katika siku hii, wanawake wote, bila kujali dini au rekodi zao za huko nyuma hushajiishwa na kuhamasishwa kuvaa vazi la stara na staha la Kiislamu la Hijabu ili kupata tajiriba na uzoefu wa siku moja ya maisha ya mwanamke Muislamu.
Licha ya kuwekwa sheria, pingamizi na vizuizi vingi dhidi ya Waislamu, makundi, wanaharakati na asasi mbalimbali za Kiislamu zinaendeleza tablighi ya kuitangaza dini tukufu ya Uislamu huko Ulaya na Marekani.../