White House yakiri, mazungumzo ya Trump na Kim Jong-Un yamefeli
(last modified Thu, 28 Feb 2019 16:03:17 GMT )
Feb 28, 2019 16:03 UTC
  • White House yakiri, mazungumzo ya Trump na Kim Jong-Un yamefeli

Msemaji wa ikulu ya Rais wa Marekani, White House amesema mazungumzo ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un yamesitishwa ghafla na kabla ya wakati wake na amekiri kwamba, hakuna makubaliano ya aina yoyote yaliyofikiwa baina ya pande hizo mbili.

 Taarifa iliyotolewa na msemaji wa White House, Sarah Sanders imesema kuwa, Rais Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un wameondoka katika kikao cha mazungumzo mjini Hanoi huko Vietnam bila ya kufikia mapatano. 

Taarifa ya White House imesema kuwa, Trump na Kim Jong-Un wamejadiliana kuhusu njia za jinsi ya kuharibiwa silaha za nyuklia na masuala ya kiuchumi lakini hawakufikia makubaliano.

Awali Sarah Sanders alikuwa amesema kuwa mazungumzo ya viongozi hao wawili yamesimamishwa ghafla.

Duru zilizokuwa karibu na mazungumzo hayo pia zimefichua kuwa, Trump na Kim Jong-Un walikatiza mazungumzo yao na kuondoka hata bila ya kushiriki katika mahfali ya chakula cha pamoja cha mchana kilichotayarishwa kwa ajili ya viongozi hao wawili.  

Tags