Bangladesh yalaani uongo wa Myanmar, yakataa kuwapokea tena Waislamu wa Rohingya
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Bangladesh amelieleza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba nchi yake haitopokea mkimbizi mwingine yeyote wa jamii ya Rohingya kutoka Myanmar.
Mohammad Shahed Alhaq, ameyasema hayo leo ambapo sambamba na kukosoa mwenendo wa serikali ya Myanmar wa kurefusha mambo na kutoa ahadi za uongo kuhusu kuwarejesha nyumbani wakimbizi Waislamu wa Rohingya, amesema kuwa, kwa sasa Bangladesh haina uwezo tena wa kupokea mkimbizi yeyote. Amezidi kubainisha kwamba sababu ya serikali ya Dhaka kuchukua uamuzi huo ni kukosekana mazingira chanya kwa ajili ya wakimbizi wa Rohingya waliopo Bangladesh.
Mohammad Shahed Alhaq ameongeza kwamba, hadi sasa hakuna mkimbizi hata mmoja aliyekwisharejea nchini Myanmar, licha ya serikali ya nchi hiyo kutoa ahadi za mara kwa mara. Itakumbukwa kuwa jeshi la Myanmar kwa kushirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kigaidi walianzisha mashambulizi ya kinyama dhidi ya Waislamu kuanzia tarehe 25 Agosti 2017 ambapo zaidi ya Waislamu elfu sita waliuawa, maelfu ya wengine kujeruhiwa na wengine karibu milioni moja kulazimika kuwa wakimbizi nchini Bangladesh.