António Guterres atahadharisha kuhusu kuzidi kuenea chuki dhidi ya Waislamu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametahadharisha kuhusu hatari ya kuenea chuki dhidi ya Waislamu duniani baada ya shambulio la kigaidi lililotokea katika misikiti miwili ya mji wa Christchurch nchini New Zealand.
Guterres alisema hayo jana (Jumanne) baada ya kuonana na Ahmad al Tayyib, Sheikh na Imam Mkuu wa Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri mjini Cairo na huku akigusia shambulio la kigaidi lililotokea tarehe 15 Machi 2019 nchini New Zealand amesema, dunia hivi sasa inashuhudia ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu.
Amesema, fikra hizo za chuki dhidi ya Waislamu zinaongezeka hivi sasa hata katika nchi za kidemokrasia sawa kabisa na katika tawala za kidikteta. Katika mazungumzo hayo, Guterres amekosoa pia fikra za kueneza chuki dhidi ya Mayahudi, za ubaguzi wa rangi na za kupiga vita wageni.
Siku ya Jumapili, António Guterres alikuweko nchini Tunisia kushiriki kikao cha 30 cha viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Arab League.
Magaidi wenye chuki za kidini walifanya mashambulizi ya kikatili tarehe 15 Machi mwaka huu katika misikiti miwili mjini Christchurch na kuua shahidi Waislamu 52 waliokuwa katika ibada ya Ijumaa na kujeruhiwa makumi ya wengine.
Mmoja wa magaidi waliofanya unyama huo aliandika katika maelezo yake binafsi kwamba ameathiriwa na fikra za kibaguzi na chuki dhidi ya Waislamu, za rais wa Marekani, Donald Trump.