Wanaharakati waandamana London, Uingereza kulaani ukatili wa Saudia
Kwa mara ya pili ndani ya wiki moja, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu wamefanya maandamano nje ya ubalozi wa Saudi Arabia katika mji mkuu wa Uingereza, London kulaani ukatili wa hivi karibuni wa watawala wa Aal-Saud dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Mamia ya wanaharakati hao wakiweo wapinzani na wakosoaji wa utawala wa Riyadh walifanya maandamano hayo jana Ijumaa nje ya ubalozi wa Saudia mjini London, wakiitaka serikali ya Uingereza na nchi nyingine za Ulaya zivunje kimya chao, mbele ya jinai hizo za kutisha za Aal-Saud.
Waandamanaji hao wamesema ukatili wa Saudia umevuka mipaka na kukanyaga sheria zote za kimataifa, na kwamba kitendo hicho cha kuwanyonga raia 37 wakiwemo watoto wadogo, mlemavu na wanazuoni, na kisha kuusulubisha mwili wa mmoja wa Waislamu hao hadharani, kinaonesha kiburi ilichonacho serikali ya Riyadh ikifahamu kuwa haitawajibishwa kwa ukatili huo.
Hii ni mara ya pili ndani ya wiki moja kwa watetezi hao za haki wa binadamu na wakosoaji wa utawala wa Aal-Saud kuandamana mjini London.
Mashirika na taasisi za kimataifa pamoja na wanaharakati wa masuala ya kijamii wanaendelea kulaani jinai ya hivi karibuni ya utawala wa Aal Saud wa Saudi Arabia ya kuwaua kwa umati raia 37 wa nchi hiyo.
Harakati za Mapambano ya Kiislamu za Hizbullah ya Lebanon na Hamas ya Palestina, shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa asasi za kimataifa zilizolaani hatua hiyo ya watawala wa Riyadh ya kutumia kisingizio cha kupambana na ugaidi kuwanyonga kwa umati Waislamu wa Kishia, zikisitiza kuwa utawala huo wa kifalme hauheshimu thamani ya utu.