Apr 29, 2019 14:29 UTC
  • 27 waua katika ufyatuaji risasi Marekani

Watu wasiopungua 91 wameuawa au kujeruhiwa katika matukio 72 ya ufyatuaji risasi katika masaa 24 yaliyopita katika maeneo tofauti ya Marekani

Ripoti iliyotolewa na Kituo cha Usajili wa Takwimu za Vitendo vya Mabavu vya Utumiaji Silaha nchini Marekani, inasema kwamba ufyatuaji risasi huo umetokea katika majimbo tofauti ya nchi hiyo ambapo umepelekea watu 27 kuuawa na wengine 64 kujeruhiwa. Ufyatuaji risasi huo umeripotiwa kutokea katika majimbo ya Pennsylvania, New York, Indiana, Ilinois, Oklahoma, Tennessee, California, South Carolina, Arizona, Louisiana na Maryland. Katika ripoti yake ya kila siku, kituo hicho cha takwimu nchini Marekani kimesema kwamba katika matukio mengine 98 yaliyoripotiwa kutokea katika kipindi cha masaa 24 ya tokea Jumamosi hadi Jumapili, katika majimbo tofautiya nchi hiyo, watu 30 walipoteza maisha yao na wengine 85 kujeruhiwa.

Wito wa kutaka matumizi mabaya ya silaha yadhibitiwe

Kila mwaka maelfu ya raia wa Marekani hupoteza maisha au kujeruhiwa katika matukio ya ufyatuaji risasi katika pembe tofauti za nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti rasmi, kuna karibu silaha za moto milioni 270 hadi 300 mikononi mwa raia wa kawaida wa Marekani, kwa maana kuwa karibu kila mtu anamiliki silaha moja nchini humo. Licha ya maombi yanayotolewa mara kwa mara na makundi ya kiraia na ya kutetea haki za binadamu kwa ajili ya kudhibitiwa silaha nchini humo lakini hakuna serikali yoyote ya Marekani iliyofanikiwa kutunga sheria za kudhibiti uuzaji wa silaha kutokana na nguvu kubwa za lobi zinazotetea umiliki wa silaha. Rais Donald Trump ni mmoja wa waungaji mkono wakubwa wa umiliki wa silaha nchini humo.

Tags