Jumuiya ya SCO yataka kuheshimiwa makubaliano ya JCPOA
(last modified Sat, 15 Jun 2019 03:45:07 GMT )
Jun 15, 2019 03:45 UTC
  • Jumuiya ya SCO yataka kuheshimiwa makubaliano ya JCPOA

Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai (SCO) imezitaka pande husika za makubaliano ya nyuklia ya Iran (JCPOA) kuheshimu na kutekeleza wajibu wao wa kufungamana na mapatano hayo ya kimataifa.

Taarifa ya kurasa 31 ya Baraza la Marais na Wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo katika mkutano uliofanyika jana Ijumaa huko Bishkek, mji mkuu wa Kyrgyzstan imesisitiza kuwa, kuendelea kufungamana na mapatano hayo ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na pande husika za makubaliano hayo.

Taarifa hiyo imekumbusha kuwa, kutekelezwa kikamilifu makubaliano hayo kunaenda sambamba na Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Hii ni katika hali ambayo, Rais Donald Trump ambaye amekuwa akiyakosoa vikali mapatano hayo ya kimataifa kwa kuyataja kuwa mapatano mabaya zaidi katika historia ya nchi hiyo, hatimaye tarehe 8 mwezi Mei mwaka uliopita alichukua hatua ya kuiondoa Marekani katika mapatano hayo muhimu ya kimataifa na wakati huohuo kuanza kutekeleza vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Iran.

Rais Donald Trump wa Marekani

Hatua hiyo ilikosolewa na kulaaniwa na nchi nyingine zilizotia saini mapatano hayo mjini Vienna mwaka 2015.

Wakati Marekani ilikuwa inaadhimisha mwaka mmoja tangu kujiondoa kwake kwenye mapatano hayo tarehe 8 mwezi uliopita wa Mei, Rais Hassan Rouhani alisema misimamo ya uoga ya nchi za Ulaya ambazo zinakwepa kutekeleza ahadi zao katika fremu ya mapatano ya JCPOA ili kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran, imeilazimisha Iran kuchukua hatua ya kupunguza ushirikiano wake kwenye JCPOA, kwa mujibu wa vipengee vya 26 na 36 vya mapatano hayo.

Tags