Walibya wamfungulia Khalifa Haftar mashitaka ya jinai za kivita
Raia wa Libya wanaoishi Marekani wamemfungulia mashitaka ya jinai za kivita kamanda muasi wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, Jenerali Khalifa Haftar wakisisitiza kuwa wapiganaji wa kamanda huyo wameua jamaa zao katika mashambulizi ya hivi karibuni ya mabomu katika mji mkuu Tripoli.
Faili hilo limewasilishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Alexandria ijimboni Virginia, ambapo walalamishi wanasema watu wa familia zao waliuawa katika hujuma za mabomu za wapiganaji wa Haftar viungani mwa mji mkuu Tripoli.
Mmoja wa raia wa Libya wanaoishi Marekani waliowasilisha faili hilo mahakamani ni Abdulhakim Tunalli mwenye umri wa miaka 59, anayesema kuwa ndugu yake Msaddek Tunalli aliuawa akiwasaidia jirani zake kuhama makazi yao baada ya kushadidi mashambulizi ya vikosi vya Haftar.
Faisal Gill, wakili wa familia zilizopoteza wapendwa wao kwenye hujuma hizo za Haftar za kutaka kudhibiti Tripoli amesema jenerali huyo anahesabiwa kuwa 'mbabe wa vita' atashitakiwa kwa kutumia uwezo na mamlaka yake kujaribu kutwaa mamlaka ya nchi. Amesema hatua itakayofuata sasa ni kukabidhiwa Haftar ilani juu ya mashitaka dhidi yake.
Jeshi la Haftar lilianza mashambulizi makali dhidi ya mji wa Tripoli tarehe 4 Aprili likisaidiwa na Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi lakini mpango wa kuteka mji huo umezimwa na kufeli.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO, mapigano hayo yamepelekea watu zaidi ya 650 kuuawa huku wengine zaidi ya 3,547 wakijeruhiwa. Aidha Umoja wa Mataifa hivi karibuni ulitangaza kuwa watu zaidi ya elfu 90 wamekimbia makazi yao huko Tripoli kutokana na kuendelea mapigano kila uchao katika mji huo.