Jul 09, 2019 03:03 UTC
  • Sera ghalati za Bin Salman zawafanya Waislamu wasusie Hijja mwaka huu

Sera ghalati na haribifu za Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia zimepelekea idadi kubwa ya Waislamu katika kona mbalimbali za dunia kutangaza kuwa hawatashiriki ibada tukufu ya Hijja mwaka huu.

Jarida la Foreign Policy la Marekani limeripoti kuwa, kushtadi ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Aal-Saud ndani na nje ya Saudia yakiwemo mauaji ya kutisha ya Jamal Khashoggi, aliyekuwa mwandishi wa habari na mkosoaji mkubwa wa utawala wa Riyadh katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul Uturuki Oktoba mwaka jana ni katika mambo yaliyowafanya Waislamu watangaze kususia Hija ya mwaka huu.

Aidha kwa mujibu wa jarida hilo, msuguano baina ya Tehran na Riyadh umechangia pakubwa kuwafanya Waislamu ambao tayari wamekwishashiriki ibada hiyo angalau mara moja maishani, kususia kushiriki tena mwaka huu.

Aprili mwaka jana, Mufti Mkuu wa Libya, Sadiq al-Ghariani aliwataka Waislamu ambao wamewashatekeleza ibada ya Hijja mara moja wasiende tena kuhiji kwani Saudia inazitumia pesa zinazotokana na ibada hiyo katika mauaji dhidi ya Waislamu jirani zao wa Yemen.

Mahujaji katika ibada ya jamarat (kumpiga shetani mawe), ikiwa ni sehemu ya amali za Hijja

Kadhalika mwaka jana, Kamati ya Kimataifa ya Uangalizi wa Usimamizi wa Saudia juu ya Ibada ya Hija ilisema kuwa, utawala wa Aal-Saud unatumia vibaya pato linalotokana na ibada ya Hija, huku ikitaka ushiriki wa asasi na serikali za Kiislamu juu ya usimamizi wa ibada hiyo tukufu na maeneo matukufu ya Haram Mbili.

Kwa kuzingatia kupanda gharama za kijeshi za Saudia katika vita vyake nchini Yemen sanjari na utawala huo kukabiliwa na nakisi kubwa ya bajeti, Riyadh imeigeuza ibada ya Hijja kuwa ingizo la pato muhimu kwa ajili ya nchi hiyo. 

 

Tags