Marekani yalegeza msimamo kuhusiana na vikwazo dhidi ya Zarif
Vyombo vya kuaminika vinasema kuwa serikali ya Marekani imeamua kulegeza msimamo na kutomuwekea vikwazo kwa sasa, Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Chanzo kimoja cha ngazi ya juu katika serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani kimenukuliwa kikisema kuwa kwa sasa serikali ya Washington imechukua uamuzi wa kutomuwekea vikwazo waziri huyo wa mambo ya nje wa Iran.
Shirika la Habari la Reuters limesema kuwa uamuzi huo wa serikali ya Washington unaonyesha kuwa imeamua kuwacha wazi mlango wa diplomasia kwa sasa kwa lengo la kuishawishi Iran iingie katika mazungumzo na serikali hiyo.
Tarehe 24 mwezi Juni uliopita, Steven Mnuchin, Waziri wa Fedha wa Marekani alichukua hatua inayokiuka wazi maazimio na sheria za kimataifa kwa kutangaza nia ya nchi hiyo ya kumuwekea vikwazo Muhammad Jawad Zarif.
Katika radiamali yake dhidi ya hatua hiyo ya Steven Mnuchin, Zarif alisema hakuwa na wasiwasi wowote kuhusiana na vikwazo hivyo kwa sababu si yeye wala familia yake wana mali wala akaunti yoyote ya benki nje ya Iran.
Akizungumza hivi karibuni na gazeti la New York Times Zarif alisema kuwa Iran tu, ndio maisha na jukumu lake la pekee.