Ujerumani yahimiza kuundwa umoja wa nchi za Ulaya wa kuwaokoa wakimbizi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54744-ujerumani_yahimiza_kuundwa_umoja_wa_nchi_za_ulaya_wa_kuwaokoa_wakimbizi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumaini amesema kuwa kuna ulazima wa kuundwa umoja wa nchi za Ulaya kwa ajili ya kuwaokoa wakimbizi na kutoa mchango wa kimsingi Berlin katika jukumu hilo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 14, 2019 02:21 UTC
  • Ujerumani yahimiza kuundwa umoja wa nchi za Ulaya wa kuwaokoa wakimbizi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumaini amesema kuwa kuna ulazima wa kuundwa umoja wa nchi za Ulaya kwa ajili ya kuwaokoa wakimbizi na kutoa mchango wa kimsingi Berlin katika jukumu hilo.

Heiko Maas alitoa mwito huo jana (Jumamosi) na kuongeza kuwa Ulaya inahitajia kuwa na umoja wa nchi ambazo zitashirikiana katika kuwasaidia na kuwaokoa wakimbizi na ambazo pia zitaweza kugawana majukumu katika jambo hilo. Amesema, Ujerumaini iko tayari kutoa mchango wa kimsingi katika kulifanikiisha suala hilo kama ambavyo inatoa dhamana ya kukubali kupokea idadi maalumu ya wakimbizi mara kwa mara. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumaini amesisitiza pia kuwa, makubaliano kuhusu opereshenei za kuwaokoa wakimbizi katika Bahari ya Mediterranean yatapelekea kufanyika zoezi la kugawana majukumu bila ya matatizo na kutamaliza misimamo ya baadhi ya nchi zinazokataa kupokea wakimbizi hao.

Jean Asselborn, Waziri wa Mambo ya Nje wa Luxembourg

 

Kabla ya hapo pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Luxembourg, Jean Asselborn, alikuwa ametaka kutekelezwa operesheni mpya za uokoaji wa wakimbizi katika Bahari ya Mediterranean kutokana na kuongezeka mno wimbi la wakimbizi wanaokimbilia barani Ulaya kutokea Libya. Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Luxembourg alizitaka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zitume haraka meli zao katika Bahari ya Mediterranean kwa ajili ya kuwaokoa wakimbizi hao.

Katika miaka ya hivi karibuni, idadi kubwa ya wakazi wa Asia Magharibi na Afrika Kaskazini wamekuwa wakitumia fukwe za Bahari ya Mediterranean kukimbilia barani Ulaya kutokana na ukosefu wa utulivu wa kiuchumi, kijamii na kisiasa katika nchi zao uliosababishwa na uingiliaji wa madola ya Magharibi katika masuala ya ndani ya nchi hizo.