Katibu Mkuu wa UN: Ubomoaji nyumba za Wapalestina si halali kisheria
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, anatiwa wasiwasi na ubomoaji nyumba za Wapalestina unaofanywa na utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa, sera za Israel za kuharibu na kuteketeza mali za Wapalestina haziendani na sheria za kimataifa.
Siku ya Jumatatu iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel, liliwatoa majumbani mwao kwa nguvu Wapalestina kadhaa na kubomoa makumi ya nyumba zao katika eneo la Wadil-Hums kusini mwa mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.
Utawala wa Kizayuni umepanga kubomoa nyumba nyingine zaidi ya 200 za Wapalestina katika mji huo wa Quds mnamo siku zijazo.
Hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni ya kubomoa nyumba za Wapalestina imelaaniwa kila pembe ya dunia, huku Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International likiitaja kuwa ni jinai ya kivita.
Utawala haramu wa Israel umekuwa kila mara ukipuuza matakwa ya Jamii ya Kimataifa na kuendeleza ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina kwa uungaji mkono na baraka kamili za Marekani.../