Familia ya binti Msomali-Muingereza aliyegharikishwa yataka haki
Familia ya binti Msomali mwenye uraia wa Uingereza aliyegharikishwa imetaka haki na uadilifu baada ya kubainika kuwa alipoteza maisha kwa njia ya kutatanisha.
Familia ya Shukri Yahya Abdi, aliyekuwa na umri wa miaka 12 imeanzisha harakati ya maandamano katika mji wa Bury nchini Uingereza baada ya binti huyo kugharikishwa katika Mto Irwill katika eneo la Greater Manchester mnamo Juni 27.
Familia ya binti huyo Muislamu, inasema aliteswa vibaya kabla ya kugharikishwa na kupoteza maisha. Aidha familia yake inasema shule aliyokuwa akisomea ya Broad Oak Sports College, imekataa kufanya uchunguzi kuhusu sababu za tukio hilo. Marehemu Shukri Abdi akiwa na familia yake walitoroka vita Somalia na kufika Uingereza kama wakimbizi kwa matumaini ya kupata eneo salama.

Familia yake imesema itaendeleza kampeni ya haki na uadilifu katika kesi hiyo huku ikisisitiza kuwa, yamkini kifo cha binti huyo kilitokana na ubaguzi wa rangi.
Takribani Waislamu milioni tatu wa Uingereza wamepitia tajiriba ya kiwango cha juu kabisa cha ubaguzi huku nchi hiyo ikishuhudia ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu.