Salehi: JCPOA sio mkataba wa upande mmoja, EU imefeli
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran (AEOI) amesema kuwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA sio mapatano ya upande mmoja, na kwamba nchi za Ulaya zimefeli kutekeleza wajibu wao wa kuyalinda mapatano hayo ya kimataifa.
Ali Akbar Salehi amesema hayo leo Jumapili katika mazungumzo yake na Cornel Feruta, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ambaye yuko safarini hapa Tehran, ambapo ameeleza bayana kuwa, "Umoja wa Ulaya ulipaswa kujaza nafasi iliyobakia wazi baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya JCPOA, lakini mpaka sasa umeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kisheria wa kuulinda muafaka huo."
Kadhalika ametetea hatua 3 ilizochukua Iran za kupunguza uwajibikaji wake kwenye makubaliano hayo, akisisitiza kuwa kitendo hicho ni sahihi na kilichofanyika katika wakati muafaka.
Feruta ambaye alimrithi Yukia Amano ambaye aliaga dunia mwezi Julai mwaka huu akiwa na umri wa miaka 72, amekutana pia na maafisa wengine wa ngazi za juu wa Iran.

Baada ya Marekani kujiondoa kinyume cha sheria katika JCPOA mnamo Mei 8 mwaka 2018, Ujerumani, Uingereza na Ufaransa ziliahidi kudhamini maslahi ya kiuchumi ya Iran katika mapatano hayo.
Mbali na kutoa matamshi ya kupinga maamuzi ya Marekani kuhusu JCPOA, nchi hizo za Ulaya hazijachukua hatua za kivitendo kutekelea ahadi zao kulinda mapatano hayo.