Mtazamo unaogongana wa Ulaya kuhusiana na JCPOA
(last modified Tue, 10 Sep 2019 07:14:13 GMT )
Sep 10, 2019 07:14 UTC
  • Mtazamo unaogongana wa Ulaya kuhusiana na JCPOA

Licha ya kuwa Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya ( Ujerumani, Ufaransa na Uingrereza) zikiwa wanachama wa kundi la 4+1 zimekuwa zikisisitiza mara kwa mara udharura wa kulindwa mapatano ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), lakini hazijaweza kuwasilisha rekodi nzuri ya utendaji wao katika uwanja huo.

Baada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutangaza siku ya Ijumaa hatua ya tatu ya kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano hayo kutokana na uvunjaji ahadi wa nchi za Ulaya, nchi hizo zimetoa radiamali ya kushangaza katika uwanja huo. Akizungumza karibuni na gazeti la Funke katika toleo lake la siku ya Jumatatu, katika kujibu hatua ya tatu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano ya JCPOA, Heiko Maas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesema: Njia ya utatuzi inaweza kupatikana lakini sisi watu wa Ulaya hatuwezi kulifanikisha jambo hilo peke yetu. Wakati huo huo Heiko Maas ametahadharisha kuhusiana na hatua hiyo ya Iran na kusema kuwa iwapo Iran haitaki kutekeleza ahadi zake kwa mujibu wa mapatano ya Vienna, jambo hilo bila shaka litatoa ujumbe ulio na makosa makubwa. Amesema, Ujerumani inaitaka Iran itekeleze kikamilifu mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015.

Jambo muhimu lililoashiriwa na afisa huyo wa ngazi za juu wa Ujerumani ni kuwa nchi za Ulaya hazina uwezo wa kulinda makubaliano ya JCPOA. Heiko Maas ameomba ushirikiano wa pande nyinginezo katika kufanikisha makubaliano hayo lakini hakuashiria ni pande gani anazozikusudia. Kwa mujibu wa ripoti kadhaa za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA, Iran imetekeleza kikamilifu ahadi zake zote ilizotoa kuhusiana na mapatano ya JCPOA, na hata hatua zake tatu  za kupunguza uwajibikaji wake katika uwanja huo zinatekelezwa kwa mujibu wa makubaliano hayo. Hivyo nchi za Ulaya hazipaswi kuitarajia Iran ifanye zaidi ya hayo.

Heiko Maas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uherumani

Heiko Maas amesisitiza kwamba mapatano sio njia ya upande mmoja. Matamshi hayo ni sahihi lakini inaonekana kuwa kiongozi huyo wa Ujerumani ameyaelewa kimakosa matamshi yake mwenyewe. Kama kweli nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani, zinataka kuyalinda makubaliano ya JCPOA zinapasa kuelekeza lawama zao kwa Marekani ambayo mwezi Mei mwaka uliopita ilijitoa kwa upande mmoja na kinyume cha sheria katika mapatano hayo ya kimataifa, na kisha kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu vikwazo vikali na vya pande zote. Hatua hiyo ilikosolewa vikali na jamii ya kimataifa zikiwemo nchi za Umoja wa Ulaya wanachama wa kundi la 4+1 ambazo zilitangaza hadharani kwamba zingebuni njia za kukabiliana na hatua hiyo ya upande mmoja ya Marekani kwa lengo la kulinda makubaliano hayo muhimu ya kimataifa.

Kwa mtazamo wa wanachama wa Mashariki wa mapatano hayo, yaani China na Russia, JCPOA ni mapatano muhimu ya kimataifa ambayo hayana mbadala. Akizungumzia suala hilo, Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alisema jana Jumatatu Septemba 9 mbele ya waandishi habari mjini Moscow akiwa na waziri mwenzake wa Ufaransa kwamba, kwa mtazamo wa Russia, hakuna mapatano mengine mbadala wa mapatano ya nyuklia na Iran yanayofahamika kama JCPOA. Kabla ya hapo, Russia ilikuwa imesema kuwa hatua ya tatu ya Iran kupunguza iwajibikaji wake katika mapatano ya JCPOA ulikuwa ujumbe muhimu kwa lengo la kuzifanya nchi za Ulaya zitekeleze majukumu yao ya JCPOA.

Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia

Pamoja na hayo, nchi za Ulaya zimethibitisha wazi kuwa licha ya kufanya juhudi zisizo na umuhimu mkubwa kama vile za kuanzisha mfumo maalumu wa kuwezesha mabadilishano ya kifedha na kibiashara na Iran mashuhuri kama Instex, lakini hazina uwezo wa kuutekeleza kutokana na kufungamana kwao kukubwa na Marekani. Jambo la kushangaza ni kuwa licha ya udhaifu huo mkubwa wa nchi za Ulaya lakini zinaitaka Iran iendelee kubakia katika JCPOA na kutekeleza kikamilifu  ahadi zake zote katika mapatano hayo. Hazijiulizi swali hili kwamba je, ni kwa nini Iran pekee ishinikizwe kutekeleza ahadi zake ilihali nchi hizo hazifanyi lolote katika kujaribu kupunguza athari mbaya za vikwazo vya Marekani dhidi ya serikali ya Tehran?

Kutokana na uzoefu wao wa huko nyuma kuhusiana na Iran, nchi za Magharibi zinatambua vyema kwamba Iran huwa huitishwi na siasa za mashinikizo wala vitisho bali kinyume chake, vitisho hivyo huwaunganisha Wairani na kuimarisha ukakamavu na umoja wao wa kitaifa kwa lengo la kukabiliana na mashinikizo ya maadui wa nje.

Tags