Trump 'alilia' Tuzo ya Nobel, asema Obama hakustahiki kupewa
(last modified Tue, 24 Sep 2019 07:48:01 GMT )
Sep 24, 2019 07:48 UTC
  • Trump 'alilia' Tuzo ya Nobel, asema Obama hakustahiki kupewa

Rais Donald Trump wa Marekani kwa mara nyingine tena amedai kuwa ana ustahiki wa kupewa Tuzo ya Amani ya Nobel.

Trump alisema hayo jana Jumatatu katika mkutano wake na Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan pambizoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kuongeza kuwa, "Ningepaswa kupewa Tuzo ya Nobel kutokana na mambo mengi sana niliyoyafanya iwapo wangeitoa tuzo hiyo kwa uadilifu, lakini hawafanyi hivyo."

Trump amekariri madai yake ya huko nyuma kwamba mtangulizi wake, Barack Obama hakupaswa kupewa tuzo hiyo. Amesema, "Walimpa Obama (tuzo hiyo) mara baada ya kuingia madarakani, na mwenyewe (Obama) hakufahamu mbona ametunukiwa tuzo hiyo. Hilo tu ndilo jambo moja ninaloafikiana na Obama."

Trump na Imran Khan pambizoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York

Obama alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2009, kwa kile kilichotajwa kama jitihada zake zisizo za kawaida za kuimarisha diplomasia ya kimataifa na ushirikiano miongoni mwa mataifa mbalimbali.

Trump amekuwa akidai mara kwa mara kuwa anapaswa kutunukiwa tuzo hiyo ya kifahari, licha ya kuandamwa na wimbi la ukosoaji nje na ndani ya nchi, kutokana na uongozi na sera zake mbovu.