Mvua na mafuriko yaua karibu watu 150 nchini India
Watu 148 wamepoteza maisha baada ya kusombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha kwa siku tano sasa nchini India.
Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, akthari ya vifo hivyo vimetokea katika jimbo la Uttar Pradesh, kaskazini mwa nchi, ambapo idadi ya walioaga dunia katika eneo hilo imeripotiwa kuwa 111.
Kadhalika makumi ya watu wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na mafuriko hayo katika eneo la Bihar, mashariki mwa India karibu na mpaka wa Nepal.
Mamlaka ya Kukabiliana na Majanga nchini humo imeripoti kuwa, watu zaidi ya elfu nne waliokolewa jana Jumatatu katika jiji la Patna, kaskazini mashariki mwa India na kupelekwa nyanda za juu. Mamlaka husika nchini India zimeripoti kuwa, yumkini idadi ya walioaga dunia kutokana na mafuriko hayo ikaongezeka, huku Idara ya Hali ya Hewa ikitoa taadhari kwa wakazi wa mji wa Mumbai wanaoishi mabondeni.

Watu zaidi ya 300 waliaga dunia nchini India katika mafuriko mengine yaliyosababishwa na kimbunga kikali cha 'Hikka'.
India ni miongoni mwa nchi ambazo hukumbwa na mafuriko kila mwaka na mamia ya watu hupoteza maisha kutokana na janga hilo la kimaumbile.