Oct 06, 2019 11:12 UTC
  • Vikwazo vya Marekani; uchokozi wa wazi dhidi ya nchi nyingine

Mashinikizo ya Marekani dhidi ya Cuba na Venezuela yanazidi kushtadi, huku nchi hizo zikiwa zinaendelea kushikamana na malengo yao na kusisitizia juu ya kuimarishwa ushikamano wao.

Katika uwanja huo, Rais Miguel Díaz-Canel wa Cuba sambamba na kuashiria kuwa nchi yake inakabiliwa na vikwazo vikali vya Marekani kwa sababu ya kuiunga mkono serikali halali ya Venezuela, amesema kuwa, vikwazo hivyo ni uchokozi wa wazi na uliopangwa mapema. Hatua hiyo imekuja baada ya Wizara ya Fedha ya Marekani kuyawekea vikwazo siku 10 zilizopita, mashirika ya usafirishaji wa baharini yenye makao yake nchini Cyprus na Panama kwa tuhuma za kukiuka vikwazo vilivyowekwa na Washington na kuzisafirishia mafuta Venezuela na Cuba. Washington imekuwa ikiituhumu mara kwa mara serikali ya Havana kuwa inaunga mkono moja kwa moja serikali ya mrengo wa kushoto ya Rais Nicolás Maduro wa Venezuela. Aidha viongozi wa Marekani wameamua kuzidisha mashinikizo dhidi ya nchi za Amerika ya Latini hususan washirika wa Venezuela, kufuatia kushindwa kwao kuiondoa madarakani serikali iliyochaguliwa kisheria ya Caracas.

Rais Miguel Díaz-Canel wa Cuba, alipoitembelea Venezuela

Kuhusiana na suala hilo Rais Miguel Díaz-Canel wa Cuba ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "Kumewekwa vikwazo vipya dhidi ya Cuba. Wanatumia uongo kushadidisha vikwazo dhidi ya Cuba. Baada ya kufeli nchini Venezuela, wameingia kwa shari nchini Cuba. Tutapambana na Marekani na tutaibuka washindi." Inafaa kuashiria kuwa, kwa miaka kadhaa sasa, Cuba imekuwa chini ya vikwazo vikali vya Marekani, hususan tangu alipoingia madarakani huko White House Rais Donald Trump. Katika uwanja huo, Trump ameziwekea mashinikizo makali Cuba, Venezuela na baadhi ya nchi za mrengo wa kushoto za Amerika ya Latini kwa lengo la kuzidhoofisha zaidi serikali za mataifa hayo na hatimaye kuziondoa madarakani. Ukweli ni kwamba kwa miaka kadhaa, viongozi wa Marekani huku wakitumia nadharia ya karne mbili zilizopita wamekuwa wakidhani kwamba wataweza kwa mara nyingine kutekeleza mkakati wa 'Monroe' kwa ajili ya kufikia malengo yao maovu katika eneo la Amerika ya Latini. Wamekuwa wakitumia mabavu na mashinikizo wakitumai kuwa watapata kupanua satwa yao katika eneo hilo. Wanaziandama nchi za mrengo wa kushito hususan za Venezuela na Cuba, ambazo ni nchi mbilizi zenye nguvu katika eneo hilo ili kwa njia hiyo ziweze kushirikiana na kutii amri za Washington. Kuwaunga mkono wapinzani wa ndani hususan wa Venezuela, kusaidia mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali halali zilizochaguliwa na wanachi na kuzidisha mashinikizo ya kiuchumi, vikwazo na vitisho vya kijeshi, ni miongoni mwa hatua za ambazo zimekuwa zikitekelezwa na Washington dhidi ya nchi hizo.

Watu wa Venezuela waliofelisha njama chafu za Marekani

Kuhusiana na suala hilo, Bruno Rodríguez Parrilla, Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba sambamba na kuashiria vikwazo vya miaka mingi vya Marekani dhidi ya nchi yake anasema: "Vikwazo hivyo vimekuwa na madhara mengi ya kibinaadamu. Licha ya kukiuka wazi haki za raia wa Cuba na hata wa Marekani yenyewe, vimekuwa na taathira nyingi hasi katika maisha ya familia za watu wa Cuba. Licha ya hayo, lakini sisi tutaendelea kusimama imara kwenye njia yetu na Marekani itafeli katika siasa zake za uhasama dhidi ya watu wa Cuba." Viongozi wa Marekani walikuwa wakidhani kuwa kama wangeweza kuiondoa madarakani serikali ya Venezuela, basi wangeweza kufungua njia ya kuitwisha ubeberu wao nchi ya Cuba na nchi nyingine za mrengo wa kushoto za Amerika ya Latini. Ni kutokana na hilo ndio maana wakaanzisha siasa za vita vyenye lengo la kumuondoa madarakani Rais Nicolás Maduro wa Venezuela, siasa ambazo hata hivyo zimeishia kugonga mwamba kutokana na mapambano ya watu wa nchi hiyo. Baada ya Washington kushindwa kumuondoa madarakani rais huyo wa Venezuela, sasa inatumia njia ya vitisho, vikwazo na mashinikizo makali dhidi ya washirika wa serikali ya Caracas, hususan Cuba. Kuhusiana na suala hilo Ernesto Limia, mwandishi maarufu wa Cuba ameandika kuwa: "Hatua mpya za Marekani dhidi ya Cuba zinahusiana na kufeli Rais Donald Trump wa Marekani huko nchini Venezuela, kwa kuwa alikuwa anataka kuiondoa madarakani serikali ya Caracas." Hata kama Washington bado inaendeleza njama za  kujaribu kuziondoa madarakani serikali za mrengo wa kushoto katika eneo la Amerika ya Latini na kisha kuziweka mahala pake serikali zinazolinda maslahi na siasa za Marekani, lakini nchi za eneo hilo zimeonyesha azma yao ya kusimama imara katika kukabiliana na siasa za mabavu za Marekani.

Tags