Ghasia zaendelea Barcelona katika maandamano ya watu wa Catalonia
Ghasia zimeendelea katika mji wa Barcelona nchini Uhispania ambapo Alhamisi jioni migahawa iliteketezwa moto baada ya maelfu kuandamana kwa amani mchana wakitaka viongozi wa eneo linalotaka kujitenga la Catalonia waachiliwe huru.
Ghasia hizo zimeendelea kwa siku nne mfululizo na zimetajwa kuwa mbaya zaidi katika miaka ya hivi karibuni Uhispania. Viongozi hao wa Catalonia wamehukumiwa vifungo virefu gerezani kutokana na kuhusika katika jitihada za mwaka 2017 za uhuru wa eneo hilo.
Kuhukumiwa kwa viongozi hao, akiwemo aliyekuwa makamu wa rais wa serikali ya jimbo hilo Oriol Junquares kumevuruga zaidi uhusiano mbaya uliopo baina ya wanaotaka kujitenga jimbo la Catalonia na serikali kuu mjini Madrid.
Vijana wakiwa wamejifunga bendera za Calatonia walikusanyika katika mji mkuu wa jimbo hilo, Barcelona, na kuandamana kwa amani. Hata hivyo maandamano hayo ya amani yaligeuka na kuwa vurugu kali katika barabra ya Rambla de Catalunya ambayo ni maarufu kwa watalii.
Taarifa zinasema zaidi ya watu 100 wamejeruhiwa kufuatia maandamano hayo ya vurugu.
Mnamo mwaka 2017, jimbo la Catalonia lilipiga kura ambayo haikuidhinishwa na serikali kuu ya Uhispania ya kutaka kujitangaza kuwa nchi huru.