Russia yasisitiza kushindwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran
Russia ikiwa mmoja wa wanachama wa kundi la 4+1 daima imekuwa ikisisitiza kulindwa mapatano ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kukosoa vikali hatua ya Marekani kuiwekea Iran vikwazo vya upande mmoja, baada ya yenyewe kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa, ikisema kuwa huo ni ukiukaji wa wazi wa Washington wa mapatano hayo.
Katika ukosoaji wa hivi karibuni, Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alisema jana Alkhamisi kwamba licha ya kuwa vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya Iran havijakuwa na natija yoyote ya maana kufikia sasa, bado vitashindwa tu katika siku zijazo. Huku akikosoa vikali vikwazo hivyo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ryabkov amesema: Msimamo huo wa Marekani bila shaka utashindwa na wala siasa hizo za nje za Marekani hazina faida yoyote. Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na nchi nyingine za dunia si halali na ni chombo cha kuzitwishwa nchi hizo matakwa ya Washington.
Sisitizo la Moscow la kushindwa kuwa na athari yoyote ya maana 'vikwazo vya kiwango cha juu zaidi' vya Washington dhidi ya Jamhuriya Kiislamu ya Iran ambavyo ilidaiwa kuwa vingeifanya Iran ibadilidhe siasa na sera zake katika eneo la Asia Magharibi, ni ishara ya wazi kwamba vimeshindwa kufikia lengo lililokusudiwa na watawala wa Marekani. Kuhusiana na suala hilo, Ryabkov anasema: Sisi tunaamini kwamba kila aina ya vikwazo vya upande mmoja ambavyo vinatekelezwa kama chambo cha siasa za nje si halali, vinapingana na sheria na kanuni za kimataifa na vinatumika kama chombo cha kufikia matakwa na siasa za kibeberu dhidi ya nchi nyingine za dunia, ikiwemo Iran.
Kwa msingi huo, kutoheshimu Marekani mapatano ya JCPOA ni moja ya dalili ambazo zimeilazimu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuchukua msimamo wa hivi sasa wa kupunguza hatua kwa hatua uwajibikaji wake katika mapatano hayo. Hii ni katika hali ambayo nchi za Ulaya nazo licha ya kutoa ahadi chungu nzima na kuanzisha mfumo usiokuwa na maana yoyote wa Instex kwa ajili ya kusahilisha miamala ya kifedha na kibiashara na Iran, lakini hazijachukua hatua yoyote ya maana ya kupunguza athari hasi zinazotokana na hatua ya Marekani ya kujitoa kwa upande mmoja katika mapatano ya JCPOA. Hilo ni jambo ambalo pia limethibitishwa na Russia ikiwa mwanachama muhimu wa mapatano ya JCPOA. Katika uwanja huo, Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameashiria mashinikizo ya Marekani dhidi ya nchi za Ulaya kuhuisiana na mapatano ya JCPOA na kusema: Nchi za Ulaya ambazo ziko chini ya mashinikizo makubwa ya Marekani zinafanya juhudi za kukwepa majukumu yao kwa kujaribu kuonyesha kwamba Iran ndio mkosa katika mzozo wa hivi sasa wa JCPOA. Marekani si tu kwamba imekiuka ahadi zake zote na kukanyaga wazi sheria za kimataifa, bali kupitia vitisho na vikwazo, inazizuia nchi nyingine za dunia kutekeleza mapatano hayo.
Huku akizitaka nchi nyingine kutotekeleza mapatano ya JCPOA kwa maslahi ya Tenran, inatoa mashinikizo na vitisho dhidi ya Iran na kuitaka itekeleza mapatano hayo bila ya kuwa na matarajio yoyote ya kunufaika nayo. Matamshi hayo ya Lavrov yanaashiria msimamo wa hivi karibuni wa nchi za Ulaya na Marekani wa kukosoa hatua ya karibuni ya Iran ya kutekeleza hatua yake ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake wa mapatano ya nyuklia baada ya kuona kuwa wanachama wengine wa mapatano hayo hawatekelezi ahadi zao. Iran imechukua hatua hiyo kwa mujibu wa vipengee viwili vya mapatano hayo ambavyo vinairuhusu kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano hayo iwapo itahisi kuwa pande nyingine hazitekelezi majukumu yao.
Ilianza kutekeleza hatua hiyo ya nne siku ya Jumatano tarehe 6 Novemba kwa kuweka gesi katika mashinepewa katika kiwanda cha nyuklia cha Fordo kwa madhumuni ya kurutubisha urani kwa kiwango cha asilimia 5.
Hatua hiyo ya Iran inathibitisha wazi msimamo wake imara wa kukabiliana na uzembeaji wa wanachama wengine wa kundi la 4+1 katika kutekeleza majukumu yao ya JCPOA na pia ni onyo kwa Marekani ambayo imekuwa ikidhani kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kutekeleza mapatano hayo bila masharti yoyote na licha ya kuwa chini mashinikizo na vikwazo vikali zaidi vya nchi hiyo ya kibeberu.
Russia imekosa vikali siasa hizo za kidhalimu na za ubabe za Marekani na kusisitiza kuwa hazikubaliki kabisa. Kwa mujibu wa Ryabkov, licha ya kuwa Wamarekani wametambua kuwa vikwazo hivyo havijakuwa na natija yoyote dhidi ya Iran kufikia sasa, lakini bado wanaendelea kutekeleza siasa hizo zilizofeli.