Korea Kaskazini: Mazungumzo yetu na Marekani yanakaribia kuvunjika kikamilifu
(last modified Sat, 09 Nov 2019 08:02:35 GMT )
Nov 09, 2019 08:02 UTC
  • Korea Kaskazini: Mazungumzo yetu na Marekani yanakaribia kuvunjika kikamilifu

Mkuu wa kitengo cha masuala ya Marekani katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini, ameelezea uwezekano wa kuvunjika kikamilifu mazungumzo kati ya Washington na Pyongyang, kutokana na ukwamishaji mambo wa Marekani.

Jo Chol-su amebainisha kwamba dirisha la fursa ya kusonga mbele mazungumzo ya nchi mbili limezidi kuwa finyu na linaelekea kufungwa kabisa. Ameongeza kuwa iwapo Washington haitochukua hatua yenye maana katika uwanja wa mazungumzo hayo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, basi yatakuwa yamefikia mkwammo kamili. Mkuu wa kitengo cha Marekani nchini Korea Kaskazini katika Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ya Asia ambaye ameshiriki mkutano wa kuzuia uenezwaji wa silaha za nyuklia mjini Moscow, Russia ameongeza kwamba serikali ya Pyongyang haipendelei kufanya mazungumzo yasiyo na faida.

Jo Chol-su, Mkuu wa kitengo cha Marekani nchini Korea Kaskazini katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini

Afisa huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini pia amesisitiza kuwa, vikwazo vya Washington dhidi ya Pyongyang, ni udhalilishaji usiokubalika na ni lazima vihitimishwe. Serikali ya Korea Kaskazini inataka kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi yake, hata hivyo Washington imekuwa ikivishadidisha vikwazo hivyo kwa visingizio tofauti.

Tags