ICC yahofishwa na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57706-icc_yahofishwa_na_jinai_za_utawala_wa_kizayuni_wa_israel
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ameelezea hofu yake kuhusu hatari za kuingizwa eneo la "Bonde la Jordan" katika sehemu ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 06, 2019 04:01 UTC
  • ICC yahofishwa na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ameelezea hofu yake kuhusu hatari za kuingizwa eneo la "Bonde la Jordan" katika sehemu ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Fatou Bensouda jana alitoa ripoti maalumu na kutangaza hofu yake kuhusu hatua iliyopangwa kuchukuliwa na Israel ya kulipora eneo la "Bonde la Jordan" la Wapalestina na kuliingiza kwenye ardhi za Palestina inazozikalia kwa mabavu.

Tangu miaka mitano nyuma, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC amekuwa akifuatilia uvamizi wa utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Kwenye ripoti yake ya mwaka huu, kama ilivyojiri kwa ripoti yake ya mwaka jana 2018, Bensouda amesema, Mahakama ya Kimataifa ya ICC imekaribia kufikia uamuzi kuhusu faili la jinai za kivita za Israel.

Kila leo Israel inapora ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

 

Ripoti ya Bensouda imetolewa siku chache baada ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kusema kwamba, katika mazungumzo yake ya simu na rais wa Marekani, Donald Trump walizungumzia uamuzi wa kutekwa na Israel eneo la "Bonde la Jordan" na kuingizwa kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Akionesha radiamali yake kuhusu jinai hiyo mpya ya Israel, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, kama utawala wa Kizayuni utaliteka eneo hilo na kuliingiza kwenye ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu, basi Mamlaka ya Ndani ya Palestina itaishitaki Israel kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC.

Juzi Jumatano pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina alilitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litekeleze sheria na maazimio ya kimataifa kupitia kukabiliana vilivyo na jinai hizo mpya za utawala wa Kizayuni wa Israel.