Russia: Vikwazo haviwezi kuchukua nafasi ya udiplomasia
(last modified Thu, 12 Dec 2019 07:49:47 GMT )
Dec 12, 2019 07:49 UTC
  • Russia: Vikwazo haviwezi kuchukua nafasi ya udiplomasia

Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema haiwezekani kupatikana amani katika Rasi ya Korea kupitia njia ya vikwazo na mashinikizo na kwamba, vikwazo haviwezi kuchukua nafasi ya udiplomasia na njia ya utatuzi wa kisiasa.

Vasily Nebenzya ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa kwa lengo la kujadili kadhia ya Korea Kaskazini na kubainisha kwamba, mwenendo wa mazungumzo ya pande mbili hauwezi kuwa na mafanikio ya kupatikana makubaliano ya pamoja hadi pale baadhi ya vikwazo vitakapofutwa. Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa ameongeza kwamba, hakuna mtu anayekubaliana na miradi ya silaha za nyuklia iliopo Korea Kaskazini, lakini pamoja na hayo suala la kuangamizwa silaha hizo hatari haliihusu tu nchi hiyo, bali eneo lote la Rasi ya Korea linatakiwa liweke hali ya kuaminiana. Vasily Nebenzya ameashiria kwamba ni suala lisilokubalika kwamba mwenendo wa vikwazo na mashinikizo pekee usaidie kufikiwa usalama na amani na kuangamiza silaha za nyuklia katika eneo hilo.

Vasily Nebenzya, Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa

Kwa ajili hiyo, mwakilishi huyo wa Russia katika Umoja wa Mataifa ametaka kupigwa hatua taratibu katika kupunguzwa vikwazo na kuirahisishia Korea Kaskazini kuweza kupata mahitaji yake ya kimaisha kama ambavyo pia amesisitiza kuchukuliwa hatua za kidiplomasia katika uwanja huo. Aidha ameitaka Marekani na nchi nyingine kujiepusha na tabia yao ya mashinikizo ya upande mmoja dhidi ya nchi nyinginezo na kusema kuwa, kitendo cha kuhalalisha vikwazo na mashinikizo dhidi ya nchi nyingine na bila kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kitendo kisichokubalika hata kidogo.

Tags