UNHCR: Watu milioni 70 duniani wamelazimika kuhama makwao
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57929-unhcr_watu_milioni_70_duniani_wamelazimika_kuhama_makwao
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNCHR) linasema zaidi ya watu milioni 70 duniani wamelazimika kuhama kutokana na vita, mizozo na mateso.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 17, 2019 04:48 UTC
  • UNHCR: Watu milioni 70  duniani wamelazimika kuhama makwao

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNCHR) linasema zaidi ya watu milioni 70 duniani wamelazimika kuhama kutokana na vita, mizozo na mateso.

Ripoti ya UNHCR imebaini kuwa, zaidi ya watu milioni 25 kati yao ni wakimbizi, wakiwa wamevuka mipaka ya kimataifa na hawana uwezo wa kurudi makwao.

Hayo yamesemwa wakati wa kuanza mkutano wa siku tatu wa dunia nzima wenye lengo la kubadilisha jinsi dunia inavyoshughulikia masuala ya wakimbizi ulioanza jana mjini Geneva, Uswisi.

Mkutano huo wa kwanza wa aina yake ambao ulianza jana mjini Geneva, Uswisi  unawaleta pamoja wakimbizi, wakuu wa nchi na serikali, viongozi wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa, mashirika ya maendeleo, wafanyabiashara na wawakilishi wa mashirika ya umma, miongoni mwa wenginie.

Kamishina Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi akiwa na wakimbizi kutoka maeneo mbali mbali duniani katika mkutano wa wakimbizi mjini Geneva, 16 Disemba 2019

UNHRC inaandaa mkutano huo kwa pamoja na Uswisi, mkutano ambao pia umeitishwa na Costa Rica, Ethiopia, Ujerumani, Pakistan na Uturuki.

Lengo la mkutano huu ni kutoa mielekeo mipya na mikakati ya muda mrefu kuwasaidia wakimbizi na jamii ambako wanaishi.

Kamishina Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema idadi ya wakimbizi imeongezeka duniani na hivyo mkutano huo wa kwanza wa dunia kuhusu wakimbizi, utajadili njia za kuwasaidia wakimbizi pamoja na nchi zinazowahifadhi.