Myanmar yawapandisha kizimbani makumi ya watoto Warohingya
(last modified Sat, 21 Dec 2019 02:43:14 GMT )
Dec 21, 2019 02:43 UTC
  • Myanmar yawapandisha kizimbani makumi ya watoto Warohingya

Watoto 23 ni miongoni mwa Waislamu wa Rohingya 93 waliofikishwa mahakamani jana Ijumaa nchini Myanmar, wakikabiliwa na mashitaka ya 'kusafiri bila vibali.'

Hata hivyo wakili wa makumi ya Waislamu hao wa jamii ya Rohingya, Thazin Myint Myat Win amesema Warohingya hao walikamatwa wakilikimbia jimbo lao la Rakhine kutokana na mauaji, dhulma na mateso wanayofanyiwa na maafisa usalama wa Myanmar wakishirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada.

Warohingya hao walikamatwa mwishoni mwa mwezi Novemba katika fukwe za Mto Irrawaddy katika jimbo la Delta, wakijaribu kutorokea nchi jirani ya Bangladesh, kwenda kujiunga na wenzao zaidi ya 740,000.

Baadhi ya watoto hao walionekana kujawa na woga na kutokana na mshtuko huo, walisikika wakilia kwa sauti mahakamani hiyo jana.

Waislamu wa Rihongya wakikimbia mauaji na mateso

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo Khin Myat Myat Tun aliwafokea watoto hao waliokua wakilia mahakamani na kuwaambia, "Nyamazeni! Hampaswi kupiga kelele wakati wa kusikilizwa kesi, vinginevyo mtapoteza haki zenu."

Wakili wa Waislamu hao wa Rohingya ameiambia mahakama kuwa, "Wateja wangu walilazmika kuyahama makazi yao jimboni Rakhine na kukimbilia usalama wao, baada ya kushadidi hali ngumu waliyokuwa wakikabiliana nayo."

Iwapo watapatikana na hatia, Waislamu hao wa Rihongya watahukumiwa kifungo cha hadi miaka miwili jela.