Uhispania yahamisha wanajeshi wake kutoka Iraq na kuwapeleka Kuwait
Uhispania imewaondoa baadhi ya wanajeshi wake huko Iraq na kuwahamishia Kuwait kufuatia jinai ya karibuni ya Marekani na kushtadi mivutano katika eneo la Asia Magharibi. Uhispania imesema imefanya hivyo kwa kuhofia usalama wa wanajeshi wake.
Naibu Waziri Mkuu wa Uhispania amesema kuwa wanajeshi wa nchi hiyo ambao walikuwa katika mazingira ya hatari wamehamishiwa nchini Kuwait na kwamba ni wanajeshi wachache tu wa nchi hiyo ndio wamesalia Iraq. Amesema Uhispania imechukua hatua hiyo baada ya kupambana moto hali ya mivutano katika eneo baada ya shambulio la kigaidi la Marekani lililomuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani Kamanda wa Kikosi cha Qods cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH).

Slovenia, Lithuania na Croatia pia zimetangaza kuwa zitaanza kuwaondoa wanajeshi wake huko Iraq kuanzia leo Alhamisi. Hiyo ni kutokana na tishio lililotolewa na Iran kwamba litalipiza kisasi damu ya Kamanda Soleimani; ambapo Iran jana alfajiri ilitekeleza sehemu ya ulipizaji kisasi hicho.
Wakati huo huo Bunge la Iraq tarehe 5 mwezi huu lilipiga kura likiunga mkono kuondoka wanajeshi wote wa kigeni nchini humo kufuatia kuuawa kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Abu Mahdi al Muhandis Naibu Mkuu wa Harakati ya Wapiganaji wa Kujitolea ya wananchi wa Iraq la al Hashd Shaabi pamoja na mashujaa wengine wa mapambano dhidi ya ugaidi.