Pakistan yaitaka jamii ya kimataifa kukomesha mauaji ya Waislamu nchini India
(last modified Sat, 14 Mar 2020 13:22:27 GMT )
Mar 14, 2020 13:22 UTC
  • Pakistan yaitaka jamii ya kimataifa kukomesha mauaji ya Waislamu nchini India

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kivitendo kusitisha mauaji ya Waislamu na ukiukaji wa wazi wa haki za binaadamu nchini India.

Aisha Farooqui ameyasema hayo katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari ambapo sambamba na kuonyesha wasi wasi wake kutokana na hali ya Waislamu nchini India, amelaani vikali ubaguzi wa kidini na ukatili dhidi ya jamii ya Waislamu wa nchi hiyo jirani. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ameongeza kwamba Islamabad inaitaka jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na asasi zote zinazojihusisha na utetezi wa haki za binaadamu, kuchukua hatua za kivitendo kwa ajili ya kusitisha mienendo iliyo kinyume cha sheria na siasa za kibaguzi za serikali ya India dhidi ya jamii ya wachache kidini wa nchi hiyo.

Ukandamizaji wa polisi dhidi ya Waislamu nchini India

Kadhalika Bi Aisha Farooqui amesema kuwa mauaji dhidi ya Waislamu yaliyofanywa na Wahindu wenye misimamo ya kufurutu ada na kadhalika kuharibiwa zaidi ya misikiti 14 katika siku nne, ni jinai iliyoratibiwa na ameitaka jamii ya kimataifa kuiwekea mashinikizo serikali ya New Delhi ili izuie maafa ya kibinaadamu. Kuendelea ghasia na mapigano ya hivi karibuni yaliyotokana na kulalamikia sheria mpya ya uraia nchini India, kwa akali Waislamu 50 waliuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. Katika uwanja huo Wahindu wenye misimamo ya kigaidi sambamba na kuwashambulia Waislamu, walibomoa misikiti huko kaskazini mashariki mwa New Delhi, huku wakiyateketeza kwa moto makazi ya Waislamu.