Sanders autaka utawala wa Trump uiondolee Iran vikwazo
Bernie Sanders, Seneta wa jimbo la Vermont anayewania kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Marekani katika uchaguzi wa mwaka huu kwa tiketi ya chama cha Democrat ameeleza kusikitishwa kwake na hatua ya utawala wa Donald Trump ya kushadidishi vikwazo dhidi ya Iran wakati huu ambapo taifa hili linakabiliana na mripuko wa ugonjwa wa Corona.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana usiku, Sanders amesema, "Iran inakabiliwa na mtikitisiko wa janga la virusi vya Corona, vikwazo vya Marekani havipaswi kuwa na mchango katika (kuzidisha) mgogoro huu wa kibinadamu."
Mwanasiasa huyo wa chama cha Democrat amesisitiza kuwa, "kama taifa tunalojali, tunapaswa kuondoa vikwazo vyote vinavyoathiri uwezo wa Iran wa kukabiliana na mgogoro huu (wa Corona), vikiwemo vikwazo vya kifedha."
Licha ya shakshia, taasisi na nchi mbali mbali duniani kuitaka Marekani iiondolee Iran vikwazo batili haswa wakati huu wa kukabiliana na Corona, lakini utawala wa Trump Jumanne iliyopita ulitangaza vikwazo vipya dhidi ya Tehran. Hivi karibuni pia, Sanders alikosoa vikali msimamo wa serikali ya Trump kuhusiana na maambukizi ya virusi vya Corona nchini humo akisema kuwa haufai, unapotosha ni hatari sana.
Donald Trump amekosolewa sana kwa kushadidisha vikwazo haswa vya madawa na vifaa vya matibabu dhidi ya taifa hili, ambalo ni katika mataifa yaliyoathiriwa zaidi na maambukizi ya virusi vya Corona duniani.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Iran, kufikia jana Jumatano, kesi za watu waliothibitishwa kuwa Corona nchini ziliongezeka na kufika 17,361, ambapo 5,710 walipata nafuu na kuruhusiwa kwenda nyumbani, huku 1,135 wakiaga dunia.