Marekani yakiri kuiwekea Iran vikwazo vya dawa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i60081-marekani_yakiri_kuiwekea_iran_vikwazo_vya_dawa
Kuendelea vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu hata katika mazingira haya magumu ya kuenea virusi vya corona na kuwekwa vizingiti vya kila aina katika njia ya kudhaminiwa vifaa vya afya na matibabu kwa ajili ya kukabiliana na virusi hivyo, kumewafanya wengi wakiri kuwa 'mashinikizo ya juu zaidi' ya Marekani dhidi ya Iran yanajumuisha hata mfumo wa afya na tiba wa nchi hii.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 31, 2020 03:49 UTC
  • Marekani yakiri kuiwekea Iran vikwazo vya dawa

Kuendelea vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu hata katika mazingira haya magumu ya kuenea virusi vya corona na kuwekwa vizingiti vya kila aina katika njia ya kudhaminiwa vifaa vya afya na matibabu kwa ajili ya kukabiliana na virusi hivyo, kumewafanya wengi wakiri kuwa 'mashinikizo ya juu zaidi' ya Marekani dhidi ya Iran yanajumuisha hata mfumo wa afya na tiba wa nchi hii.

Vyombo vya habari vya Marekani pia vinakiri ukweli huo mchungu. Kuhusu hilo, gazeti la Marekani la Washington Post liliandika Jumapili kwamba vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vinazuia vifaa vya tiba na vilevile malighafi ya uzalishaji dawa kufikishwa nchini Iran. Katika ripoti yake, gazeti hilo linasema: Vikwazo vya kulemaza vya Marekani dhidi ya mfumo wa kibenki na uuzaji nje mafuta ya Iran vimepunguza pakubwa uwezo wa Iran kujidhaminia fedha za kununulia bidhaa za dharura, yakiwemo madawa na malighafi ya kutengenezea vifaa vya kuyazalisha.

Vikwazo hivyo visivyo vya kibinadamu vinatekelezwa katika fremu ya siasa za Marekani za mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuiondoa nchi yake katika mkataba wa kimataifa wa nishati ya nyuklia mashuhuri kwa jina la Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), mwezi Mei 2018, serikaliya Washington ilianzisha tena vikwazo vyake vya kidhalimu dhidi ya Iran vilivyokuwa vimesimamishwa kwa muda wakati wa kufanyika mazungmzo hayo. Tokea wakati huo Marekani imekuwa ikiiwekea Iran na katika nyakati tofauti, vikwazo vikali na eti vya kulemaza ambavyo vimejumuisha sekta zote zikiwemo za uchumi, biashara, mafuta, madini na hata vyombo vya mahakama na kidiplomasia humu nchini.

Trump akitangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran

Nukta muhimu hapa ni kwamba vikwazo hivyo pia vimejumuisha bidhaa za kibinadamu zikiwemo za afya, tiba na madawa, jambo ambalo limepelekea mamia ya Wairani kupoteza maisha kutokana na kutopata vifaa vya dharura vya kuokoa maisha. Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amedai kwamba nchi hiyo haijaiwekea Iran vikwazo vya bidhaa za kibinadamu katika hali ambayo vikwazo hivyo kivitendo vimeyazuia mashirika ya nchi za Magharibi kufanya biashara na Iran.

Pamoja na hayo, kuenea virusi vya corona duniani kumedhihirisha upande mwingine mweusi wa mashinikizo ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, suala ambalo limeifanya nchi hii ikabiliwe na matatizo makubwa katika kudhamini vifaa vya dharura vya kitiba kwa ajili ya kuokoa maisha ya wanadamu na kuzuia kuenea virusi hatari vya corona. Washington inadai kwamba imechukua baadhi ya hatua kwa lengo la kurahisisha ununuzi na utumwaji wa vifaa vya matibabu nchini Iran, lakini kinyume na madai hayo mmoja wa mawakili wanaoshughulikia vikwazo katika idara ya kudhibiti madawa katika Wizara ya Fedha ya Marekani anasema: Hatua hizo haziondoi marufuku dhidi ya bidhaa za dharura (za kibinadamu) dhidi ya Iran. Amesema kutekelezwa hatua hizo kuhusu vikwazo vya Marekani ni mfano wa kutembea kwenye uwanja uliojaa mabomu ya kutegwa ardhini.

Pompeo anayetoa madai ya uongo kuhusu kuruhusu bidhaa za kibinadamu kuingia Iran

Kufikia sasa, Umoja wa Mataifa, baadhi ya nchi, taasisi muhimu za kimataifa na hata mashirika na wanasheria wa Marekani wameitaka serikali ya Trump isimamishe kwa muda vikwazo hivyo visivyo vya kibinadamu dhidi ya Iran katika mazingira magumu ya hivi sasa ya kuenea virusi hatari vya corona, lakini White House imekataa katakata ombi hilo na kusisitiza  kuendelea kutoa mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran ili kuifanya ikubaliane na matakwa yake ya kibabe. Si tu kwamba Washington imekataa kujibu wito huo wa kimataifa bali imeendelea kuiwekea Iran vikwazo vipya, ikitarajia kuwa huenda ikafanikiwa kuipigisha magoti. Bila shaka hiyo ni ndoto ya watawala wa Marekani ambayo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, haitathibiti.